Katika kona ya kusini mwa Tanzania, katikati ya mji wa kihistoria wa Songea mkoani Ruvuma, kuna hazina ya dhahabu isiyo na thamani ya fedha bali ya kumbukumbu,utu na uzalendo.
Makumbusho ya Kumbukumbu ya Dkt. Rashid Mfaume Kawawa, maarufu kwa jina la heshima "Simba wa Vita", kiongozi aliyesimama imara kama ngome ya utaifa na ukombozi wa Afrika.
Makumbusho haya, yaliyofunguliwa rasmi tarehe 27 Februari, mwaka 2017, ni tawi la Makumbusho ya Taifa la Tanzania na yanapatikana katika Mtaa wa Kawawa, eneo la Bombambili, Manispaa ya Songea. Mahali hapa si tu panahifadhi historia ya mtu mmoja, bali ni mlango wa kuingia katika historia ya taifa zima na harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Kumbukumbu Zinazoishi Ndani ya Kuta Zake
Ndani ya makumbusho haya, historia haiandikwi kwa kalamu tu, bali inaishi katika vitabu, mavazi, medali, picha za kihistoria na samani alizotumia Hayati Dkt. Kawawa katika maisha yake binafsi na ya kisiasa.
Moja ya vivutio vikubwa zaidi ni uwepo wa nyumba ya kisiri iliyo na handaki (njia ya maficho), iliyotumiwa wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Handaki hilo linaeleza kimya kimya, kwa sauti ya historia, namna kiongozi huyu alivyokuwa kiungo muhimu katika mikakati ya kisiasa na kijeshi wakati wa enzi ya ukoloni.
Kawawa na Filamu za Kwanza za Kiafrika Nchini Tanzania
Katika historia ya filamu barani Afrika, wengi hawawezi kudhani kuwa jina la Dkt. Rashid Kawawa lingehusishwa na uigizaji lakini ndilo linaloongoza ukurasa wa kwanza.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa, Philipo Maligisu, Kawawa alikuwa Mtanzania wa kwanza kuigiza na kutengeneza filamu za Kiafrika.
Filamu ya kwanza, "Muhogo Mchungu" ya mwaka 1951, ndiyo ilimtambulisha kwa mara ya kwanza katika uigizaji, ikiwa ni kazi iliyotayarishwa kwa lugha ya Kiswahili yenye dhamira ya kupigania utu na haki. Baada ya filamu hiyo, aliigiza kazi nyingine kama:
Kwa jumla, Kawawa alishiriki katika angalau filamu tano zilizoweka msingi wa tasnia ya filamu ya Kiafrika hapa nchini.
Makumbusho Ambayo Ni Chuo cha Uzalendo
Makumbusho haya si tu mahali pa kutembele bali ni darasa la uzalendo, chimbuko la maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Hapa, historia haikai kwenye vitabu bali huonekana, hushikika na huhisiwa.
Watoto wa shule, wanafunzi wa vyuo, watafiti wa historia, na watalii wa ndani na nje ya nchi hupata fursa ya kujifunza siasa, utamaduni, na mapambano ya ukombozi kupitia maisha ya mtu mmoja aliyeweka maslahi ya taifa mbele ya yake binafsi.
Kwa mujibu wa takwimu za Makumbusho ya Taifa, zaidi ya 8,000 ya wageni walitembelea makumbusho haya kati ya mwaka 2021 na 2024, idadi ambayo inaendelea kupanda mwaka hadi mwaka, ikiwa ni ishara tosha ya ongezeko la shauku ya Watanzania na wageni kuhusu historia yao.
Historia Inapovuta Uhai Upya Songea
Katika dunia ya leo yenye kasi kubwa ya maisha na teknolojia, Makumbusho ya Dkt. Rashid Mfaume Kawawa ni kioo cha kale kinachoakisi maadili ya sasa. Ni mwaliko wa kutafakari, kujifunza na kujivunia historia ya taifa letu.
Hili ni taji la kumbukumbu lililojaa utukufu, na kwa yeyote anayetafuta kuelewa maana ya uongozi wa kweli, uzalendo wa dhati, na thamani ya kujitolea kwa ajili ya nchi Makumbusho ya Kawawa ni sehemu ambayo lazima ufike.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.