Shirika la Hilali Nyekundu ya Uturuki (Turkish Red Crescent) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) limekabidhi mradi wa visima vitano katika Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, ukilenga kuwapunguzia wananchi adha ya maji na kuwapatia huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi visima hivyo iliyofanyika katika shule ya Sekondari ya Mkako, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameyashukuru mashirika hayo kwa kujitoa na kuchimba visima hivyo ili kuwasaidia wananchi kupata maji na kuwawezesha kufanya shughuli zingine za kujipatia kipato.
Ameahidi kulinda visima hivyo ili viendelee kutumika kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. Amesema serikali imefanya kazi kubwa katika sekta ya maji, lakini bado kuna uhitaji mkubwa, hivyo ameliomba Shirika la Hilali Nyekundu ya Uturuki kuendelea kushirikiana na serikali katika maeneo mengine ili kupunguza changamoto kwa wananchi.
Kwa upande wake, Rais wa Turkish Red Crescent, Profesa Dr. Fatma Meriç Yılmaz, amesema maji si rasilimali ya asili tu bali ni uhai wenyewe. Amesisitiza kuwa mradi huo unawapa wananchi fursa ya kupata maji safi, kulinda afya na kuchangia ustawi wa jamii, huku akieleza kuwa ni alama ya urafiki na mshikamano kutoka kwa watu wa Uturuki kwa Tanzania.
Rais wa Red Cross Tanzania, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile, amesema uchimbaji wa visima hivyo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 400. Amesema visima vitano vimechimbwa katika shule za msingi tatu na sekondari mbili, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi.
Naye Rais wa Red Cross Mkoa wa Ruvuma, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Mhe. Judith Kapinga, amesema mradi huo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa kijiji cha Mkako, kwani eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa ya maji kwa muda mrefu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.