Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Gasper Makondo, amewataka watumishi wa halmashauri zote za mkoa huo kuboresha huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa PEPMIS/e-Utendaji kwa watumishi wa sekta ya afya na elimu, yaliyofanyika katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea, Makondo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha mifumo ya kidigitali inarahisisha utendaji kazi na kuongeza uwajibikaji.
Ameeleza kuwa ingawa mfumo wa PEPMIS umekuwa ukitumika, mara kadhaa changamoto za utekelezaji na matumizi yake zimejitokeza. Hata hivyo, viongozi na watumishi sasa wamekusudia kubadilika na kuendana na matarajio ya wananchi kwa kufanya maboresho makubwa zaidi katika nyanja zote za huduma.
Bi. Makondo amewasihi washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia kama chachu ya kuboresha huduma kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa uratibu mzuri wa mafunzo hayo ili kuhakikisha yanawafikia watumishi wote wa halmashauri na kuleta matokeo chanya katika sekta husika.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na huduma bora kwa wateja (customer care) ili kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa serikali.
Naye Mratibu wa Mfumo wa e Utendaji, Bw. Oswin Mkinga, amesema kuwa baada ya kufanya uchambuzi wa matumizi ya mfumo huo, imebainika kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho.
Amebainisha kuwa mafunzo hayo kwa watumishi yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wa umma ili waweze kutumia mfumo kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.