Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed, ameagiza kusimamishwa kazi mkandarasi wa Kampuni ya Bogeta Engineering Ltd anayesimamia mradi wa ujenzi wa madarasa, mabweni na vyoo katika Shule ya Sekondari Jenista Mhagama, Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Katika ziara yake ya kukagua miradi ya elimu, RC Ahmed amesema mkandarasi huyo asimamishwe mara moja na kutafutwa mkandarasi mwingine atakayetekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba na kuzingatia kasi inayotakiwa na Serikali. Mradi huo unahusisha mabweni mawili, madarasa sita na matundu kumi ya vyoo kwa gharama ya shilingi milioni 417.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Amali ya Lundusi, RC Ahmed ameagiza Halmashauri husika kuangalia namna ya kujenga mabweni katika shule hiyo ili kuwasaidia wanafunzi kujisomea kwa utulivu pindi itakapoanza kutoa masomo kwa wanafunzi.
Akihitimisha ziara yake katika Shule ya Msingi Mnyonga, ambako amekagua ukarabati wa madarasa, ujenzi wa madarasa mapya na vyoo, RC Ahmed amesisitiza miradi yote inayotekelezwa katika mkoa kuwa na mpango kazi utakaosaidia kuonyesha hali halisi ya utekelezaji, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi ili wajue miradi hiyo inavyotekelezwa.
Pamoja na mambo menginge ameonya kuwa miradi ikitekelezwa bila kuzingatia taarifa ya Makadirio ya Kiasi cha Kazi (Bill of Quantities (BOQ) haiwezi kukidhi viwango, hivyo wasimamizi wanapaswa kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana moja kwa moja katika ubora wa miradi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.