Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha za wazazi inaonekana.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua programu ya elimu ya kujitegemea na miradi mbalimbali shuleni hapo, Brigedia Jenerali Ahmed amesema kwa kuwa wazazi wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa katika miradi hiyo, iwapo thamani ya michango yao haitadhihirika, wazazi wanaweza kukata tamaa na kushindwa kujitokeza kuchangia miradi mingine kwa siku za usoni.
Katika hatua nyingine ameipongeza shule hiyo kwa kuanzisha programu ya elimu ya kujitegemea. Akisisitiza bila juhudi hizo shule inaweza kukwama kwa kutegemea fedha za serikali pekee, ambazo mara nyingine hazitoshi kutatua changamoto zinazojitokeza.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Teresa Mlwilo, amesema taasisi hiyo ina miradi minne ya kujitegemea. Miradi hiyo ni mashine ya kukoboa na kusaga nafaka pamoja na kuongeza virutubishi, ufyatuaji wa tofali, kilimo cha mahindi na ujenzi wa uzio wa shule.
Amefafanua kuwa wazazi walichangia zaidi ya shilingi milioni 14 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka pamoja na mashine ya kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi. Kwa sasa, wazazi wanaendelea kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.