Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amefanya ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe katika kampuni za Ruvuma Coal na Jitegee, zilizopo Wilaya ya Mbinga.
Ziara hiyo imelenga kuona maendeleo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea mkoani humo na kulinganisha hali ya uzalishaji na mwelekeo wa soko la dunia ambalo kwa sasa inaelezwa kuwa limeporomoka, hali inayochangia kupunguza mapato ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika ziara hiyo, Brigedia Jenerali Ahmed amesema anakubaliana na wawekezaji kuwa kushuka kwa soko la dunia kunatokana na kupungua kwa uhitaji wa makaa ya mawe. Hata hivyo, amesisitiza kuwa kampuni hizo zina nguvu kazi ya kutosha na mitambo ya kisasa, hivyo shughuli za uchimbaji zinaendelea kama kawaida.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amesema anaungana na wananchi wa Ruvuma kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya barabara hususan kipande cha Kitai hadi Ruanda. Amesema barabara hiyo ikikamilika itapunguza changamoto za usafiri na usafirishaji wa makaa ya mawe, na hivyo kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Amebainisha changamoto kadhaa zilizotolewa na wawekezaji, ikiwemo masoko ya makaa ya mawe ambapo amewashauri wawekezaji kuendelea kutafuta masoko ya kimataifa na ya ndani ya nchi badala ya kusubiri wateja pekee.
Brigedia Jenerali Ahmed ameongeza kuwa Serikali itashughulikia changamoto zinazohitaji uingiliaji wake, ikiwemo ujenzi wa barabara ili kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe ili mradi huo uwe na tija kwa mkoa na taifa kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.