Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa shukrani za dhati kwa viongozi na wananchi wa mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi, akieleza kuwa mchango wao umekuwa nguzo muhimu katika kupandishwa kwake cheo kutoka Kanali hadi Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akizungumza katika hafla maalum ya pongezi iliyoandaliwa kwa heshima yake kufuatia uamuzi huo uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Brigedia Jenerali Ahmed amesema cheo hicho si tu heshima kwake binafsi, bali ni fahari kwa viongozi na wananchi wa mkoa mzima wa Ruvuma.
"Ninaomba niwahakikishie kupandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali ni heshima kubwa ambayo si yangu pekee yangu, Bali ni ya wananchi na viongozi wote wa Mkoa wa Ruvuma mlioendelea kushirikiana nami kwa mshikamano, nidhamu na upendo mkubwa," alisema Brig. Jen. Ahmed.
Ameeleza jinsi ambavyo amekuwa akijivunia kufanya kazi na wakuu wa wilaya wa mkoa huo, akiwataja kuwa ni watendaji mahiri wanaomwezesha katika mafanikio ya kiutawala ndani ya mkoa, akiwaomba waendelee kumshika mkono na kufanya kazi kwa bidii na moyo wa uzalendo kama ilivyokuwa awali.
Vilevile Brigedia Jenerali Ahmed hakusita kuishukuru familia yake kwa uvumilivu na msaada waliompatia katika kipindi chote ambapo amekuwa akitumika serikalini na jeshini, akisema kuwa mafanikio hayo ni matunda ya uvumilivu wa familia.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amemwelezea Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed kama kiongozi mwenye hekima, maarifa na uadilifu wa hali ya juu, akisema uongozi wake umechochea mshikamano miongoni mwa watumishi wa umma na kuboresha mazingira ya kazi kwa kiwango kikubwa.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.