Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amezindua rasmi Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara Mkoa wa Ruvuma chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), likiwa na lengo la kuwatambua, kuwawezesha, na kuwalea wafanyabiashara wadogo ili waingie katika mfumo rasmi wa kodi baada ya kukua kiuchumi.
Akizungumza katika viwanja vya Soko Kuu mjini Songea, wakati wa uzinduzi wa dawati hilo Brig. Jen. Ahmed amesema kuwa sekta isiyo rasmi inatoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni saba na kuchangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la Taifa.
Hata hivyo, ameeleza kuwa bado idadi kubwa ya wafanyabiashara hao ambao wapo katika sekta isiyo rasmi wamebaki nje ya mfumo rasmi wa kodi, jambo linalopunguza uwezo wa serikali kukusanya mapato na kudhoofisha jitihada za kukuza uchumi wa Taifa.
Amebainisha kuwa ili kuwaingiza wafanyabiashara wadogo katika mfumo wa ulipaji kodi, ni lazima kuwatengenezea mazingira rafiki ambapo sasa dawati hili litatoa elimu ya biashara na kuwasaidia kutambua fursa za maendeleo na kuimarika kiuchumi kwa mtu binafsi, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine ameahidi kushirikiana kwa karibu na mameneja wa TRA mkoani Ruvuma kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanasikilizwa, wanapewa makadirio sahihi ya kodi kulingana na ukubwa wa biashara zao, mazingira yenye haki na usawa.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma, Ndg. Nicodemus Mwakilembe, amefafanua kuwa lengo la dawati hilo si kuwatoza kodi wafanyabiashara wadogo kwa sasa, bali ni kuwawezesha kwa kuwapa elimu ya namna ya kuendesha biashara endelevu huku wakiunganishwa na taasisi mbalimbali za kifedha na kisheria ili kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.