Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema serikali ya mkoa huo imeamua kuchukua mkakati mahususi na wa vitendo wa kupambana na tatizo la udumavu kwa kuunganisha sekta za kilimo, lishe na elimu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mkakati wa kuendeleza zao la soya kilichofanyika katika ukumbi wa Songea Club, mjini Songea, Brigedia Jenerali Ahmed amesema mkakati huo unalenga kuhamasisha matumizi ya maziwa ya soya kama sehemu ya kuboresha lishe na kuhakikisha wanafunzi wa shule za awali na msingi wanapata maziwa ya soya kupitia mpango wa lishe shuleni.
"Zao la soya ni la kimkakati katika mkoa wetu, lenye protini nyingi, ubora wa hali ya juu na lenye madini muhimu pamoja na mafuta yenye afya. Zao la soya ni rahisi kuandaa, gharama nafuu na linaweza kuzalishwa kwa kutumia malighafi inayopatikana ndani ya mkoa. Soya si suluhisho la lishe pekee bali ni fursa ya kiuchumi," alisema Brig. Jen. Ahmed.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi Mary Gasper Makondo, ameeleza kuwa katika miaka ya karibuni uzalishaji wa zao la soya umeshuka, licha ya umuhimu wake mkubwa katika kuboresha lishe ya jamii.
Amesema zao hilo ni miongoni mwa mikakati ya mkoa katika kukabiliana na udumavu na kudumisha lishe bora kwa watoto, wanawake na wananchi kwa ujumla.
Naye Katibu Mtendaji Mkuu wa MCODE, Ndg. Ahsante Zenda, amesema kuwa kupitia mradi wa zao la soya, taasisi hiyo inalenga kupunguza changamoto za lishe kwa jamii ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuongeza tija katika uzalishaji wa soya shambani, sambamba na kuboresha afya ya lishe kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.