Sekta ya afya mkoani Ruvuma imepiga hatua kubwa kutokana na jitihada za serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua ambazo zimeongeza matumaini kwa maelfu ya wananchi wanaotegemea huduma bora za afya.
Akizungumza na wanahabari,mjini Songea Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dr. Louis Chomboko, alisema uwekezaji katika miundombinu, rasilimali watu na huduma za msingi umeibadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya afya ya mkoa huo.
“Wananchi sasa wanashuhudia huduma bora zaidi, upatikanaji wa dawa umeongezeka na teknolojia imewekwa ili kurahisisha huduma,” alisema.
Kwa sasa,mkoa wa Ruvuma ina jumla ya vituo 473 vya huduma za afya, vikiwemo hospitali 18, vituo vya afya 50 na zahanati 341. Serikali inamiliki sehemu kubwa ya vituo hivyo, ikiwa na hospitali 9, vituo vya afya 39 na zahanati 277.
Katika maboresho ya teknolojia, mfumo wa GoTHOMIS,Dr.Chomboko alisema umesimikwa kwenye vituo 192 kati ya 325 vya afya, sawa na asilimia 64.74, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji huduma.
Hata hivyo amesema Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nao umeimarika kwa kiwango kikubwa, kutoka asilimia 50 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2024. Serikali imetumia shilingi bilioni 7.95 kuhakikisha upatikanaji wa dawa, huku asilimia 90.1 ya mahitaji yakifikiwa kwa ufanisi.
Amesema Huduma za chanjo zimepata mafanikio makubwa, ambapo chanjo ya kifua kikuu (BCG) imefikia asilimia 166 ya malengo, polio asilimia 135 na HPV asilimia 126. Aidha, jumla ya vituo 348 vinatoa huduma za afya ya uzazi na mtoto, kati yake vituo 325 vikitoa chanjo na 313 vikitoa huduma za kujifungua.
Kulingana na Mganga Mkuu huyo wa Mkoa,Katika mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, wanawake 22,718 walichunguzwa, 301 (sawa na asilimia 1.3) waligundulika kuwa na VIA positive na 87% walitibiwa. Aidha, wanawake 79 walihisiwa kuwa na saratani na kupatiwa rufaa kwa uchunguzi zaidi.
Ameongeza kuwa Huduma za ustawi wa jamii kupitia mpango wa iCHF pia zimeimarika. Watoto 283,094 wameandikishwa, sawa na asilimia 119.9 ya lengo, huku kaya 31,767 zikijiunga na mfuko huo kwa kuchangia shilingi milioni 953.
Mkoa pia umepokea vifaa vipya vya uchunguzi, vikiwemo mashine 27 za hematolojia, 26 za biochemistry, mashine 9 za Genexpert na mashine 8 za X-ray za kidijitali zilizogawiwa kwenye hospitali mbalimbali.
Kwa upande wa miundombinu, Dr.Chomboko amesema zaidi ya shilingi bilioni 4.76 zimetumika kwenye miradi 29 ya afya, miradi miwili ikikamilika kwa asilimia 100 na mingine 27 ikiwa katika hatua mbalimbali za umaliziaji. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, zaidi ya shilingi bilioni 3.42 zimetengwa kwa miradi mipya.
Mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga sekta ya afya imara, endelevu na inayomfikia kila Mtanzania, hususan wananchi wa mikoa ya pembezoni kama Ruvuma.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.