Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema serikali inatambua umuhimu wa mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya Mbambabay kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi huo, Profesa Mbarawa amesema bandari hiyo inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 80 inatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2026. Akisisitiza kuwa serikali itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, kwa kuwa wananchi wa ukanda huo wameisubiri bandari hiyo kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa katika usanifu wa bandari hiyo, mabadiliko ya tabianchi yamezingatiwa kwa kipindi cha miaka 50 ijayo, hivyo hakutakuwa na changamoto hata iwapo kiwango cha maji katika Ziwa Nyasa kitaongezeka au kupungua.
Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amebainisha kuwa wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria watalipwa mara baada ya uhakiki kukamilika, kwani tathmini tayari imefanyika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema bandari hiyo itakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa wananchi mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.
Ameeleza kuwa bandari hiyo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa gharama nafuu, kufungua fursa za biashara za kikanda na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na ushuru.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mheshimiwa John Nchimbi, amesema changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa jimbo hilo ni ratiba ya meli, ambazo kwa sasa hufanya safari mara mbili tu kwa mwezi. Amemuomba Waziri wa Uchukuzi kulifanyia kazi suala hilo ili kurahisisha usafiri na shughuli za wananchi wa Jimbo la Nyasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.