Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mheshimiwa Kapenjama Ndile, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameongoza maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa kituo cha watoto yatima cha SWACCO, kilichopo katika Manispaa ya Songea.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Ndile amesisitiza kuwa thamani ya maisha ya binadamu haipimwi kwa mali, utajiri au vyeo, bali kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wengine, hasa wale wasiojiweza, akitoa mfano wa Hayati Regina Chinguku, mwanzilishi wa kituo hicho, ambaye alijitoa kwa moyo kuwahudumia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Ndile amewahimiza watoto waliowahi kulelewa na wanaoendelea kulelewa katika kituo hicho kutokata tamaa kutokana na changamoto walizopitia akiwakumbusha kuwa Mwenyezi Mungu ameandaa fursa nyingi za mafanikio kwa kila mmoja wao, hivyo ni muhimu kuzitumia kwa bidii badala ya kulalamika au kunung’unika.
Vilevile amewataka kujituma ili waweze kufikia mafanikio na hatimaye kuwasaidia wengine, akisisitiza kuwa wao pia wana uwezo wa kufanya mageuzi makubwa katika jamii, ikiwemo kuanzisha vituo vingine vya kulea watoto yatima kama walivyosaidiwa wao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo cha SWACCO, Bi. Anna Eric Mgenya, amesema dhamira ya kituo hicho ni kutoa elimu kwa jamii ili kukomesha mimba za utotoni, maambukizi ya VVU, unyanyapaa, ongezeko la umaskini na watoto wa mitaani.
Bi. Anna pia ameeleza changamoto zilizopo katika kituo hicho, ambazo ni ukosefu wa bwalo la chakula, hali inayowalazimu watoto kula na kujisomea ndani ya mabweni. Pia, uhaba wa mabweni umekuwa kikwazo katika kupokea watoto wapya wanaohitaji msaada.
Licha ya changamoto hizo, SWACCO imekuwa ikiwajengea uwezo watoto wake kwa kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo kama kilimo na ufugaji, ili kuepuka utegemezi wa kila kitu, hata hivyo, kituo kinakabiliwa na ukosefu wa teknolojia za kisasa katika utekelezaji wa shughuli hizo.
Naye Jane Turuka, mmoja wa watoto waliowahi kulelewa katika kituo hicho, ametoa ushuhuda wa mafanikio yake akisema alipokuwa SWACCO aliishi maisha yenye heshima, alivalishwa, alisomeshwa na hatimaye kufikia elimu ya shahada ya saikolojia, hivyo amewashukuru wafadhili wote kwa mchango wao katika maisha ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.