Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, imeweka historia mpya kupitia utekelezaji wa Siku za Lishe katika vijiji mbalimbali, hatua iliyobadili maisha ya maelfu ya wananchi hususan watoto na akina mama wajawazito.
Takwimu zinaonesha zaidi ya watoto 12,000 chini ya miaka 5 walipimwa katika robo ya pili ya mwaka huu na visa vya utapiamlo kupungua kwa asilimia 18 ikilinganishwa na mwaka 2022. Vilevile, akina mama zaidi ya 7,500 wamepata huduma za chanjo, elimu ya unyonyeshaji na mbinu bora za kuandaa chakula chenye virutubisho.
Afisa Lishe wa Wilaya ya Tunduru, Martine Kigosi, amesema mpango huo umeleta mapinduzi ya uelewa wa jamii. Kupitia elimu ya bustani za mbogamboga, familia zaidi ya 1,200 tayari zimeanzisha mashamba madogo ya mboga, hali inayoongeza upatikanaji wa chakula chenye madini na vitamini majumbani.
Wananchi nao wameshuhudia mabadiliko. “Nilijifunza jinsi ya kuchanganya nafaka, mboga na kunde. Mtoto wangu sasa anapata uzito vizuri,” amesema Mwajuma Hassan wa Kijiji cha Matemanga.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watoto 3 kati ya 10 nchini Tanzania bado wanakabiliwa na udumavu. Hata hivyo, mfano wa mafanikio ya Tunduru unatajwa kuwa dira ya kitaifa kupunguza udumavu chini ya asilimia 25 ifikapo mwaka 2030.
#LisheBora #AfyaKwanza #TunduruYajivunia #GenerationStrong #SDG2030
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.