Ni mbuga chache za wanyama pori hapa nchini ambazo zimebahatika kuwa na maingilio au mapitio ya wanyama ambayo yanaitwa ushoroba kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine jirani .
Pori la wanyamapori Liparamba lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa mapori yaliyopitiwa na ushoroba wa wanyama.
Afisa Utalii wa Pori hilo Maajabu Mbogo amesema pori hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2000,limebahatika kuwa na wanyamapori wakubwa na wadogo wakiwemo tembo,simba, chuo,viboko,mamba,tandala,pofu,palahala,kuro,nyati, pundamilia,fisi,chui na mbweha na ndege kama vile kanga, koribustard(Mbawala) na fundichuma.
“Neno liparamba ni la kabila la kimatengo ambao ni wenyeji wanaoishi wilaya ya Mbinga,maana liparamba ni mbuzimawe,pori hili lina makundi makubwa ya tembo,ambao ni wakimbizi kwa sababu huwa wanatoka Msumbiji na kuhamia Liparamba’’,alisema Mbogo.
Amesema makundi makubwa ya tembo kutoka Msumbiji yanaingia kwa wingi katika pori la Liparamba kuanzia mwezi Machi kila mwaka na kufikia mwezi Julai,tembo wanaanza kurudi nchini Msumbiji na kwamba inapofika kati ya Septemba na Oktoba wanabaki tembo wachache sana ndani ya hifadhi hiyo.
“Inapotokea kule nchini Msumbiji majangili yamewashambulia tembo au kuwasumbua,tembo hao wanapoingia katika hifadhi ya Liparamba hawatoki,wanabaki ndani ya pori la Liparamba kati ya miaka miwili hadi mitatu bila kutoka na kurudi Msumbiji kwa sababu Liparamba ni sehemu salama ya kuishi tembo’’,alisisitiza.
Amesema katika pori la Liparamba pia amewahi kuonekana simba mweupe na kwamba jambo hilo sio kitu cha ajabu kwa kuwa viumbe hai wakiwemo wanyama na mimea ikipata kasoro kwenye ngozi au majani inaweza kuwa na rangi nyeupe.
Anavitaja vivutio vingine vilivyopo katika pori hilo ni uwepo wa aina mbalimbali za nyoka kama vile jamii ya mamba na kobra na kwamba pori hilo limepitiwa na mito 25 yakiwemo maporomoko ya maji ya Nakatuta katika Mto Ruvuma ambayo ni kivutio cha asili cha utalii.
Kwa mujibu wa Afisa Utalii huyo,pori hilo lina vivutio vinavyofaa kufanya utalii wa kupanda kwenye mawe kwa sababu ndani ya hifadhi hiyo,kuna mawe makubwa yanayofaa kwa utalii wa aina hiyo.
Amesema ndani ya pori hilo kuna miti ya ajabu ukiwemo mti wa mtetereka ambao ukikauka unabadilika na kuwa jiwe na kwamba miti ya aina hiyo ipo kwa wingi katika eneo la Nakatuta kandokando mwa Mto Ruvuma hivyo kuvutia watalii wengi wanaopenda kufanya utafiti wa miti na mimea.
Katika eneo la Mkuyu ndani ya pori la Liparamba pia kuna kivutio kinachowashangaza wengi ambacho,maji yanayotiririka kwenye mto Mkuyu yametengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba.
“Maji yameweza kutengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba,ukichukua ramani ya Afrika na kuangalia ramani iliyotengenezwa na maji hakuna tofauti ni ramani kabisa ya Afrika,haya ni moja ya maajabu katika pori la Liparamba’’,alisema Mbogo.
Kwa upande wake Mhifadhi Msaidizi wa pori hilo Paul Protas anakitaja kivutio kingine kilichopo katika pori hilo ni uwepo wa ndege aina ya koribustard(Mbawala) ambaye hapa nchini anatumika kama alama ya Taifa kama ilivyo kwa mnayama twiga.
“Huyu ni ndege mkubwa ana uwezo wa kufikisha uzito KG 16,ana urefu wa SM 1330,huyu ni ndege wa kitaifa,anachinjwa kwa kibali kinachoombwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’,anasisitiza.
Pori la akiba Liparamba lina muunganiko wa moja kwa moja na ziwa Nyasa hivyo mtalii akimaliza kuangalia vivutio vya utalii ndani ya pori la Akiba Liparamba anaendelea na utalii kupitia milima ya Livingistone ambayo imeshuka moja kwa moja kwende Bonde la ufa hadi ziwa Nyasa.
Afisa Utalii wa Pori la Akiba Liparamba Maajabu Mbogo anasema ukitoka Liparamba unashuka na milima ya Livingstone ambayo ni maarufu duniani ma kukutana na ziwa Nyasa lenye vivutio lukuki vya utalii.
“Hili ni ziwa adimu duniani,ni benki ya vivutio vya utalii,lina aina zaidi ya 400 za samaki wa mapambo,lina fukwe za asili za kuvutia,visiwa vya kuvutia,eneo la ziwa Nyasa ndiyo eneo pekee duniani ambalo mabonde mawili ya ufa la mashariki na Magharibi yamekutana’’alisema Mbogo.
Hata hivyo amesema maeneo ya milima ya Livingstone kando mwa ziwa Nyasa ndiyo ,maeneo ambayo ndege wahamiaji toka bara la Ulaya na maeneo mengine duniani wanapumzika kabla ya kuendelea na safari.
Utafiti umebaini kuwa Liparamba ni eneo kipekee duniani lililopo katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo lenye msitu mnene wa asili na wenye mandhari ya kuvutia .
Makala imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 26.2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.