Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ametoa wito kwa vijana wa mkoa huo kuchangamkia kwa umakini na weledi fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa wa Ruvuma, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kufikiwa bila ushiriki wa vijana wenye maono na uthubutu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana wa Mkoa wa Ruvuma lililofanyika katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea, Brigedia Jenerali Ahmed amesema vijana wana jukumu kubwa la kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo cha kisasa, kuongeza thamani ya mazao, pamoja na kuchangamkia fursa za biashara katika maeneo ya mipakani na ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya upatikanaji wa mitaji, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi ili kuwawezesha vijana. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio haya yatakuwa na maana endapo vijana wataamua kushiriki kikamilifu na kubeba jukumu la maendeleo.
Brigedia Jenerali Ahmed Abbas ameeleza kuwa nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na kidigitali, hivyo Taifa linahitaji vijana wenye nidhamu ya kazi, ubunifu, uadilifu na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amesema kijana anaweza kufikia nafasi yoyote katika jamii endapo atakuwa mwaminifu, makini, na mwenye kujituma akisisitiza kuwa jukumu la viongozi ni kuhakikisha vijana wanajengewa mazingira bora ya kufanikisha ndoto zao.
Naye Katibu wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Ruvuma, Gervas Komba, ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya maendeleo kuanzia ngazi za chini.
Kwa upande mwingine mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Zuberi Yassin, ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na vijana kwa kusikiliza changamoto zao, hususan katika upatikanaji wa mikopo na mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.