Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema kuwa wazee wa Tanzania wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa, mchango ambao umewezesha nchi kufikia hatua ya maendeleo ya sasa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Manispaa ya Songea, Mkoani Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed amesisitiza kuwa mchango wa wazee haupaswi kusahaulika, bali kuenziwa na kuigwa na vizazi vya sasa.
Amesema katika makumbusho ya vita vya maji maji kuna historia inayotoa somo muhimu kwa vijana wa kizazi cha sasa, ikikumbusha kuwa wazee wa Taifa hili walitimiza wajibu wao kwa kujitoa muhanga kwa ajili ya ustawi wa vizazi vijavyo, hivyo jukumu la kuendeleza amani, kudumisha maendeleo na kuimarisha ustawi wa jamii sasa limehamia mikononi mwa vijana na wananchi wa sasa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Amon Mpanju, ameeleza kuwa wazee si tu hazina ya Taifa, bali ni nguzo muhimu katika ustawi wa jamii.
Amesema Wazee wamekuwa walinzi wa imani, mila na tamaduni katika Taifa, hivyo Wizara itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazee, kuenzi mchango wao, kuwathamini na kuhakikisha wanatoa mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, Mzee David Sendo, amesisitiza umuhimu wa jamii kutambua na kuthamini utu wa kila mtu, akitoa rai kwa jamii kuacha vitendo vya kudhalilishana, kudharauliana, kunyanyasana na hata kuua, akisema kuwa kila mtu ana haki sawa.
Ameongeza kuwa uonevu na ukatili dhidi ya wazee na makundi mengine ni changamoto inayopaswa kujadiliwa na kutafutiwa suluhisho kwa kuwa Wazee wanahitaji dunia yenye utulivu na amani.
Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa wazee na kuhamasisha jamii kuendelea kuwajali, kwa kutambua kuwa wao ni rasilimali kuu ya Taifa la Tanzania.

Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.