Ni umbali wa kilometa nane tu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, lakini Bustani ya Ruhila ni safari ya kipekee kuelekea kwenye utulivu, asili na mandhari ya kupendeza isiyo na mfano. Hii si bustani ya kawaida—ni hazina ya utalii wa wanyamapori inayokua kwa kasi chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Kanda ya Kusini Mashariki.
Asili ya Ruhila inarutubishwa na historia ya zaidi ya nusu karne ya uhifadhi. Tangu mwaka 1973 hadi sasa, eneo hili limepitia mikononi mwa mamlaka mbalimbali hadi kufikia usimamizi wa TAWA mwaka 2017, hatua iliyofungua ukurasa mpya wa uwekezaji wa kisasa katika sekta ya utalii mkoani Ruvuma.
Ofisa Mhifadhi wa TAWA, Daudi Tesha, anasimulia kuwa jina "Ruhila" lilitokana na mto wenye maporomoko ya kihistoria uliowahi kusababisha watu wengi “kuhira” au kuzama — hatimaye likazaliwa jina Ruhila. Mto huo unapita katikati ya bustani, ukiupa uzuri wa asili unaovutia.
Ndani ya Ruhila Zoo kuna aina mbalimbali za wanyama walioachwa huru wakiwemo pundamilia, nyumbu, pofu, swala pala, digidigi na kuro. Aidha, wanyama wakali kama simba, chui na tembo wamewekwa kwenye vizuizi maalum, hali inayowezesha wageni kuwaona kwa usalama.
Bustani imezungukwa na uoto wa asili wa miti ya miyombo, misukusuku na mipangapanga ambayo imehifadhiwa kwa zaidi ya miaka 50 bila kuharibiwa. Mazingira haya yanaiweka Ruhila kuwa bustani pekee ya mji yenye uzuri wa pori la kweli.
Ruhila si sehemu ya kuangalia tu wanyama. Imeboreshwa kwa huduma zinazowafanya wageni kuifurahia bustani hiyo kwa njia nyingi zaidi. Vibanda vya kupumzika, bwawa la kuogelea, michezo ya watoto, baskeli na magari madogo yanayozunguka bustani yote ni sehemu ya burudani zinazopatikana.
Aidha, eneo maalum la kupiga kambi lina miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano—likiwa salama na rafiki kwa watalii. Kiingilio ni cha kawaida: Sh 5,900 kwa watoto na Sh 11,800 kwa watu wazima.
Fursa za uwekezaji ni nyingi. Kutoka kwa hoteli, huduma za chakula na vinywaji, hadi uwekezaji wa kambi za mahema kando ya Mto Ruhila. Hata miundombinu ya utalii wa kutembea kwa kutumia vitoroli vya waya imepangwa kuanzishwa kutokana na bonde na miti mikubwa inayozunguka eneo hilo.
Kwa mujibu wa Tesha, TAWA ina mpango wa kuongeza idadi ya wanyama wa kupendezesha zaidi bustani, akiwemo twiga, mbuni na swala wanaoweza kuingiliana kwa karibu na watalii—ikiwemo kupigwa nao picha na kuwalisha.
Aidha, vizimba vya kutembea vinavyobeba wanyama vinaandaliwa kwa ajili ya kuwafikia watu wasio na muda wa kuitembelea bustani moja kwa moja.
Lakini zaidi ya yote, ni mshikamano wa jamii ya Songea unaoifanya Ruhila kuwa kivutio salama na endelevu. “Wananchi wamekuwa walinzi wakuu wa rasilimali hii. Tunawashukuru kwa moyo wa uzalendo wa kweli,” anasema Tesha.
Kwa mipango na uwekezaji unaofanyika, Ruhila Zoo iko mbioni kuwa kivutio kikuu cha Afrika Mashariki. Ndoto ya Tesha ni kuiona Ruhila ikitajwa Kigali, Kampala, Nairobi, hata Paris. Ni ndoto inayowezekana ikiwa juhudi za serikali, wawekezaji, na jamii zitaungana kwa pamoja.
Ruhila si tu bustani—ni urithi hai wa Songea unaohitaji kuenziwa, kutembelewa na kuwekewa nguvu mpya kila siku. Karibu Ruhila, penye pumzi ya asili, sauti za wanyama, na ahadi ya uzuri usioisha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.