KIKOSI cha askari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kanda ya kusini kituo cha Kalulu,kimeweka kambi maalum katika kijiji cha Milonde wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ili kusaidia kufukuza wanyama wakali na waharibifu hususani Tembo wanaotoka kwenye hifadhi na kuvamia makazi ya watu.
Askari hao watahusika kufukuza Tembo katika vijiji vya Changarawe,Namwinyu,Kajima,Kalulu,Milonde na Matemanga ambavyo vimekuwa na matukio ya wananchi kuvamiwa na Tembo mara kwa mara wakiwa katika shughuli zao.
Afisa Uhusiano wa Tanapa kituo cha Kalulu mkoani Ruvuma Stephen Mpondo amesema,kazi kubwa itakayofanywa na askari hao ni kuzuia Tembo kabla hawajafika kwenye mashamba ya wananchi na kuwarudisha kwenye maeneo yao.
Amesema,askari wataendelea kuwepo katika kijiji hicho kwa muda mrefu ili kuhakikisha wananchi wanabaki salama na wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali hasa kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo.
Amewataka wananchi na viongozi wa vijiji hivyo,kuhakikisha wanatoa taarifa haraka mara tu wanyama wanapovamia kwenye mashamba yao kabla hawajafanya uharibifu wa kula mazao.
Mpondo amewaomba wananchi,kuwapa ushirikiano askari ili waweze kutekeleza majukumu yao hasa ikizingatia kufukuza Tembo au wanyama wengine hatari siyo jambo rahisi na jepesi kunahitaji watu wenye uthubutu na waliopata mafunzo ya namna ya kukabiliana na wanyama hao.
Afisa wanyamapori wa wilaya ya Tunduru Dunia Almasi amesema,kwa muda mrefu Tembo wamekuwa wasumbufu kwa kuvamia mashamba na kufanya uharibifu wa kula mazao,kujeruhi na hata kuuwa.
Kwa mujibu wa Almasi,licha ya serikali kupitia Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere kupeleka askari,wanaendelea kutoa elimu ya kuzuia na kufukuza wanyama hao kwa kutumia uzio wa pilipili,matofali ya pilipili na mabomu baridi.
Amesema,kutumia uzio wa pilipili ni njia sahihi kwani baadhi ya vijiji ambavyo wananchi wamepatiwa mafunzo na elimu hiyo matukio ya Tembo kuvamia mashamba na makazi ya binadamu yamepungua kwa kiwango kikubwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.