WANANCHI wa kata ya Matemanga wilayani Tunduru,wamewaomba makarani waliopewa kazi katika zoezi la sensa ya watu na makazi,kuharakisha kuuliza maswali na kuchukua taarifa za kaya ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali badala ya kukaa muda mrefu majumbani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,licha ya zoezi hilo kupokelewa vizuri lakini changamoto kubwa ni makarani ambao wanatumia muda mrefu kufanya mahojiano na kujaza taarifa za kaya,hivyo kusababisha baadhi yao kushindwa kusubiri.
Askofu wa kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (Kiuma)wilayani humo Noel Mbawala alisema,muda wanaotumia makarani kujaza taarifa ya kaya moja kwenye vishikwambi ni mrefu ambapo ameshauri makarani hao kuongeza kasi ili kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
Alisema kutokana na majukumu ya wananchi katika kujitafutia ridhiki,ni vyema makarani wakaongeza bidii ya kazi ili watu wapate muda wa kwenda kwenye shughuli zao za kiuchumi na sio kukaa muda mrefu wakisubiri kuhesabiwa.
“zoezi hili la sensa linalofanyika ni zuri sana kwa maslahi ya nchi na taasisi yetu ya Kiuma,hata hivyo tunawaomba sana makarani waongeze spidi ya kujaza taarifa wanapofika kwenye kaya”alisema Askofu Mbawala.
Aidha,ameipongeza Serikali kwa kuratibu vyema zoezi hilo kwani linatekelezwa kisasa ikilinganishwa na sensa zilizopita na litatoa fursa kwa serikali yetu kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Hata hivyo alisema,zoezi la sensa la mwaka huu liko tofauti na miaka ya nyuma kwani maswali mengi yanayoulizwa na makarani yanalenga kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Askofu Mbawala,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwani tangu ilipoingia madarakani imefanikiwa kutekeleza na kusimamia miradi mingi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hali iliyowezesha wananchi kujikita katika kazi za kujiongezea kipato badala ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kijamii mbali na makazi yao.
Hawa Athuman mkazi wa Milonde, alitaja changamoto ya zoezi hilo ni muda mrefu unaotumika kufanya mahojiano kwenye kaya moja yenye idadi kubwa ya watu na maswali yanayoulizwa na makarani ni mengi.
Fulko Hyera,amefurahishwa na hatua ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuandaa zoezi la sensa kwa mwaka 2022.
Alisema,wananchi wana matumaini makubwa kwa serikali yao kwani baada ya kupata takwimu na idadi sahihi ya watu itaboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa baadhi ya maeneo hapa nchini.
“baada ya zoezi hili,sasa serikali inaweza kujua kwa idadi ya watu waliopo wanahitaji maji kiasi gani,pembejeo za kilimo kiasi gani na huduma nyingine za kijamii ambazo zitatolewa kulingana na idadi ya wananchi wa eneo husika”alisema Hyera.Kwa upande wake Afisa wa sensa kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu anayesimamia tarafa ya Matemanga Nassoro Shamte alisema, kwa ujumla zoezi hilo linakwenda vizuri kutokana na hamasa kubwa iliyofanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali.
Alieleza kuwa, zoezi la sensa katika tarafa ya Matemanga linaenda vizuri kutokana na idadi kubwa ya watu kuelimishwa na wao kufahamu kuhusu umuhimu wa zoezi hilo ambalo linafanyika kila baada ya miaka kumi hapa nchini.
Akizungumzia kuhusu changamoto hiyo Shamte alisema,viongozi na makarani wamejipanga vizuri ili kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa na kuwatoa hofu wale ambao hawajahesabiwa kuwa makarani watawafikia katika makazi yao.
Naye karani wa sensa Isaya Kalaliche alieleza kuwa,zoezi hilo limekuwa rahisi kwao kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi wa vitongoji waliopo kwenye maeneo waliyopangiwa kwa ajili ya kuhesabu watu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.