BENKI ya NMB imeweza kutoa msaada wa madawati na viti vyenye thamani ya shilingi milioni 15 katika shule tatu wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Msaada huo umekabidhiwa na NMB kwa Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Peter Ntalamka katika hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari Kipapa.
Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo,Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amezitaja shule ambazo zimepata msaada huo kuwa ni shule ya msingi Luposo iliyopata madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni tano.
Shule nyingine amezitaja kuwa ni shule ya sekondari Kiamili ambayo imepata msaada wa viti 50 na meza 50 vyenye thamani ya shilingi milioni tano na shule ya sekondari ya Kipapa ambayo imepewa msaada wa viti 50 na meza 50 vyenye thamani ya shilingi milioni tano.
“Vifaa hivi ambavyo tunavikabidhi leo,ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na sisi kama benki inayoongoza Tanzania,tunaowajibu wa kuhakikisha jamii inayotuzunguka inafaidika kutokana na faida tunayopata’’,alisisitiza Shango.
Hata hivyo Meneja huyo wa Kanda ya Kusini,amesema kwa miaka kadhaa sasa Benki ya NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita Zaidi kwenye miradi ya elimu na afya ambako imekuwa inatoa madawati,vifaa vya kuezekea,vitanda na magodoro yake Pamoja na kusaidia majanga yanapotokea nchini.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Aziza Mangasongo ambaye aliwakilishwa na Peter Ntalamka ameipongeza NMB kwa kutoa msaada huo kwa shule tatu za Wilaya hiyo ambapo amesema msaada huo utasaidia kuboresha taaluma kwa wanafunzi.
Amesema Benki ya NMB imekuwa kila mwaka inatoa misaada mbalimbali katika shule za Wilaya ya Mbinga ambapo mwaka jana ilisaidia vifaa vya kuezekea bweni lenye thamani ya shilingi milioni 80 katika shule ya sekondari Litembo.
Naye Mkuu wa shule ya sekondari ya Kiamili Mary Ndunguru akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada wa viti na meza kutoka NMB,ameipongeza Benki hiyo kwa kutatua changamoto ambazo zilikuwa zinaikabili shule hiyo.
Amesema shule yake yenye wanafunzi Zaidi ya 1000,kabla ya NMB kutoa msaada huyo ilikuwa na upungufu wa meza na viti Zaidi ya 300 ambapo hivi sasa changamoto ya wanafunzi wawili kukaa kiti kimoja imepungua,hata hivyo ametoa rai kwa NMB kuendelea kutoa msaada katika shule kwa sababu changamoto bado zipo.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa shule ya sekondari Kipapa Flora Komba akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake,ameipongeza NMB kwa msaada huo ambao amesema umepunguza changamoto ya viti na meza kwa wanafunzi.
NMB ndiyo Benki ambayo imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100,ikiwa na matawi 226 na ikiwa na idadi ya wateja Zaidi ya milioni nne.
Imeandikwa na Albano Midelo
Mbinga
Julai 5,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.