Watumishi wa Serikali Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kujiridhisha na taarifa za taasisi zinazotoa mikopo kabla ya kuchukua mikopo kutoka katika taasisi husika.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo katika kikao kazi kilichohusisha walimu, watendaji wa Kata pamoja na taasisi za mikopo zilizopo Wilayani Mbinga.
Mangosongo ameeleza kuwa kumekuwa na migogoro kati ya taasisi za mikopo pamoja na watumishi ambao ndio wakopaji adha ambayo inaathiri utendaji kazi wa watumishi hao.
Ameitaja moja ya sababu ya migogoro hiyo ni watumishi kuchukua mikopo kiholela bila kuwa na taarifa sahihi za taasisi hizo na kupelekea baadhi yao kutapeliwa fedha zao au kukatwa makato makubwa tofauti na makubaliano.
"Kuna taasisi za magumashi unaenda pale anakusainisha mkataba hakupi na akikupa mkataba wa kimagumashi na wewe una haraka ya hela mkataba husomi matokeo yake unatapeliwa" Amesema Mangosongo
Hata hivyo Mangosongo amewataka watumishi hao kujikita katika shughuli za kiuchumi na sio kutegemea mshahara pekee hali inayopelekea kujiingiza katika mikopo na kushindwa kulipa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Andrew Mbunda amebainisha kuwa kikao kazi hiko kinakwenda kuleta matokeo chanya na kubadilisha fikra za watumishi hao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.