HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imechangia Zaidi ya shilingi milioni 240 kwenye mfuko wa wanawake wa uwezeshaji vijana na wenye ulemavu.
Akizungumza kwenye kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG kwa mwaka 2020/2021 kwenye ukumbi wa Sekondari ya Kigonsera,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge imeipongeza Halmashauri ya Mbinga kwa kuchangia kwa asilimia 92 kwenye mfuko huo wenye vikundi 13.
Kati ya fedha hizo kundi la wanawake limepata Zaidi ya shilingi milioni 108,vijana Zaidi ya shilingi milioni 106 na kundi la wenye ulemavu ni shilingi milioni 25.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,pia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kuweza kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 77 ya lengo la kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni nne ambapo Halmashauri hiyo imeweza kukusanya Zaidi ya shilingi bilioni tatu.
“Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hamkufikia kile kiwango cha angalau asilimia 81 hivyo nawapa hongera kwa kiasi,lakini nawatia shime ongezeni jitihada za kukusanya na kuhakikisha Halmashauri yenu inafikia lengo la kitaifa la kukusanya kuanzia asilimia 81’’,alisisitiza RC Ibuge.
Hata hivyo Ibuge amesema licha ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2020/2021,mwenendo wa hati za ukaguzi kwa Halmashauri hiyo kwa miaka minne mfululizo unaonesha kuwa wamekuwa wanapata hati safi kuanzia mwaka 2017/2018 hadi mwaka 2020/2021.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho ameipongeza serikali kwa kutoa fedha Zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza mradi wa jengo la Halmashauri hiyo ambalo linatarajia kukamilika hivi karibuni.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita imekuwa inajitahidi kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma kwa asilimia 100 ambapo amesisitiza viongozi kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Juni 15,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.