BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la Bunge la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Novemba19, 2019 ambapo Rais Dkt.John Magufuli, aliweka sahihi kwenye Tangazo la kuanzisha rasmi Hifadhi hiyo.
Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ina ukubwa wa kilometa za mraba 30,893 na kuifanya kuwa moja ya hifadhi kubwa duniani yenye vivutio vingi vya asili na wanyamapori wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere inayounganisha Mikoa minne ya Ruvuma, Pwani , Lindi na Morogoro.
Mndeme anasema Hifadhi hiyo imetokana na Pori la Akiba la Selous na kwamba Katika Mkoa wa Ruvuma hifadhi hiyo inapatikana katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.
“Tunamshukuru na kumpongeza sana Mhe. Rais kwa kuanzisha hifadhi ya Nyerere ndani ya Mkoa wetu, itaenda kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi ndani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla’’,anasisitiza Mndeme.
Mndeme anabainisha zaidi kuwa katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kuna wanyama wengi wakiwemo Simba, Tembo, Twiga, Chui, Nyati, mbwa mwitu na wengine wengi ambao ni vivutio vikubwa vya utalii.
Kulingana na Mndeme uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere una faida nyingi katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Kufungua utalii katika ukanda wa kusini na hivyo kuchochea shughuli za utalii katika Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Faida nyingine za Hifadhi ya Taifa ya Nyerere anazitaja kuwa ni kutangaza vivutio vingine vya utalii vilivyopo ndani ya Mkoa wa Ruvuma ndani na nje ya Mipaka ya nchi yetu yaTanzania na itasaidia katika kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla kutokana na shughuli za kitalii.
Anabainisha zaidi kuwa hifadhi hiyo,itasaidia katika kutangaza na kuongeza fursa za uwekezaji katika fukwe za Ziwa Nyasa kutokana na mwingiliano utakaokuwepo wa watalii wanaoingia na kutangaza vivutio vya Simba weupe na Tembo wakimbizi katika hifadhi ya Liparamba.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 28,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.