NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa David Silinde ameagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa na Watanzania kuzitumia kumbukumbu na historia za Kitaifa kuwa chanzo cha ajira ili kuendelea kupigana vita dhidi ya umasikini.
Mheshimiwa Silinde ametoa maagizo hayo wakati anazungumza kwenye kilele cha kumbukizi ya miaka 115 ya Mashujaa wa vita ya Majimaji mjini Songea.
Ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuhakikisha kuwa historia ya Taifa letu inatumika kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi ,hivyo ametoa wito kwa vijana kutathmini na kuthamini utamaduni wetu na kutumia nguvu zao katika kulinda Utalii na kujiletea maendeleo.
Hata hivyo amesema haitakuwa na maana yoyote tukisema kuwa tunawaenzi na kuenzi tamaduni zetu wakati maadili tunayorithi kutoka kwa mababu zetu yanaendelea kuporomoka na kupotea hivyo amesisitiza kujitoa kwao muhanga kuendelee kujidhihirisha kwetu kama ilivyo Kauli Mbiu ya mwaka huu Utamaduni wetu, nguvu zetu kwa Maendeleo ya Utalii na Uchumi Wetu.
‘’Naomba niwakumbushe kuwa njia nzuri Zaidi na ya pekee ya kuendelea kuwaenzi Mashujaa hawa ni kuhifadhi tamaduni zetu kwa kufanya kazi kwa bidii, kulinda rasilimali za Taifa, kupambana na kuzuia rushwa, ujangili wa wanyama pori na madawa ya kulevya’’ amesema Silinde.
Kwa upande wake Chifu wa tano wa Wangoni Emanuel Zulu amemuomba Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho Tanzania kuwa tunapoombeleza kifo cha Mashujaa wa Vita ya Majimaji tuanze kwa kuwakumbuka wahanga wote wa Vita ya Majimaji kuanzia Kilwa mkoani Lindi kwa tarehe zao na kumalizia mkoani Ruvuma .
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema akitoa salamu za Mkoa ametoa rai kila mwananchi kujiandaa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajia kufanyika Agosti mwaka huu , pia amekumbusha umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa hiari kupata chanjo ya UVIKO 19.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Kutoka ofisi ya Habari ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
28 Februari 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.