Viongozi na Wataalamu kutoka Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe wamefanya ziara ya mafunzo ya ukusanyaji mapato kupitia shughuli za uchimbaji makaa ya mawe katika wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Wataalam hao kutoka Ileje wameongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bi. Farida Mgomi na Menejimenti ya Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Haji Juma aliwaongoza wageni hao kutembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Kampuni ya Jitegemee Holdings uliopo Kijiji cha Ntunduwaro, Kata ya Ruanda pia wageni hao walitembelea katika eneo la kuchakata na kuuzia makaa ya mawe la Kampuni ya Jitegemee lililopo Kijiji cha Paradiso.
Wataalamu hao pia walitembelea kituo cha ukaguzi na ukusanyaji wa mapato kutokana na makaa ya mawe katika bandari ya nchi kavu Kitai ambapo walijifunza namna Halmashauri hiyo inavyosimamia makusanyo ya ushuru, tozo na mapato mbalimbali yanayotokana na makaa ya mawe.
Biashara ya makaa ya mawe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeleta mafanikio makubwa ambapo katika mgodi mmoja tu wa Jitegemee umeweza kutoa ajira za kudumu 85,ajira za muda 150 na serikali kuingiza mapato mbalimbali kutokana na ushuru na tozo mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kupata mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi kwa niaba ya Menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Ileje aliwashukuru viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa mafunzo waliyopata katika ziara hiyo ambayo amesisitiza yataimarisha ukusanyaji wa ushuru na mapato kupitia sekta ya makaa ya mawe katika wilaya ya Ileje.
Biashara ya madini ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma imeshamiri baada ya mauzo jumla ya makaa ya mawe ya tani 450,675.32 ndani ya nchi na tani 1,060,699.05 ziliuzwa nje ya nchi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022.
katika Mkoa wa Ruvuma,kuna jumla ya kampuni 14 za wachimbaji Makaa ya Mawe na kwamba katika Mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha Madini ya Makaa ya Mawe kilichouzwa ni jumla ya tani 639,482.55 ziliuzwa ndani ya nchi na tani 837,846.29 ziliuzwa nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema Kwa kipindi cha hivi karibuni Mkoa wa Ruvuma umeweza kuvutia na kupata wawekezaji wengi waliowekeza kwenye shughuli zinazohusiana na madini ya Makaa ya Mawe kama Uchimbaji, Ununuzi, Usafirishaji na Uchenjuaji.
Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Mei 25,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.