Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe, amesema uongezaji wa virutubishi kwenye chakula unalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata chakula bora na chenye lishe kwa afya na maendeleo endelevu ya nchi.
Ameyasema hayo wakati akisoma hotuba katika uzinduzi wa kanauni za urutubishaji wa chakula za mwaka 2024 na makabidhiano ya mashine za urutubishaji chakula uliofanyika kitaifa katika ukumbi wa Chandamali manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Amesema uongezaji virutubishi kwenye chakula ni mkakati unaofanyika duniani kote kama njia madhubuti ya kupambana na utapiamlo au magonjwa yanayotokana na upungufu wa Vitamini na Madini, kama vile watoto kuzaliwa na tatizo la kichwa kujaa maji, mgongo wazi na mdomo sungura.
Amesema Serikali imejihakikishia kuwepo kwa teknolojia za uongezaji virutubishi na kuweka mazingira rafiki kwa wazalishaji wote wa chakula ili kufanikisha zoezi, ametoa rai kwa wazalishaji wa unga wa mahindi na ngano na wadau wengine wote kuendelea kurutubisha chakula.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, amesema pamoja na juhudi za kuongeza idadi za mashine za kuongeza mashine za urutubishaji, mkoa wa Ruvuma bado unakabiliwa na changamoto ya uelewa na mwitikio mdogo jamii kuhusu umuhimu wa chakula kilichoongezewa virutubishi au vitamin na madini.
Ametoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kanuni za urutubishaji chakula ili zilete matokeo mazuri katika kukabiliana na hali duni ya lishe.
Kwa upande wake mwakilishi wa Waziri wa Afya, Dkt. Saitori Laizer, amesema urutubishaji wa chakula utachochea kupungua kwa kasi vifo vya kina mama wajawazito na wanaojifungua pamoja na watoto wanaozaliwa kwa ajili ya kukosa kinga ya mwili na upungufu wa damu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.