barabara ya kisasa ya lami kutoka Kitai, kupitia Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi imeanza kuandikwa katika sura mpya ya maendeleo ya kusini mwa Tanzania.
Huu si mradi wa kawaida wa ujenzi wa barabara; ni dira ya matumaini kwa maelfu ya wananchi wanaoishi na kutegemea ukanda huu wa kimkakati.
Mradi huu unaolenga kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 95, ni sehemu ya ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha miundombinu ya usafiri ili kuunganisha kwa urahisi maeneo ya ndani na bandari za Ziwa Nyasa, na hivyo kufungua milango ya uchumi, biashara, na utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Bilioni 155 kutekeleza mradi huu
Kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 155, Serikali imeweka mkazo mkubwa si tu katika kujenga barabara, bali katika kujenga maisha mapya kwa wananchi.
Mkandarasi aliyeteuliwa, kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), anaendelea na kazi, akitekeleza mradi huu kwa awamu mbili ,awamu ya kwanza kutoka Amanimakolo hadi Ruanda yenye urefu wa kilomita 35, na awamu ya pili kutoka Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi yenye urefu wa kilomita 50.
Tayari, kufikia Machi 2025,TANROADS Mkoa wa Ruvuma imeanza rasmi ujenzi wa awamu ya pili.
Barabara Inayoleta Maisha
Kwa wakulima wa kahawa, mahindi, na mazao mengine ya biashara kutoka Mbinga, barabara hii inamaanisha soko la haraka. Kwa wavuvi na wafanyabiashara wa Ndumbi, ni tumaini la mzunguko wa bidhaa na wateja.
Kwa wajasiriamali wa utalii, ni fursa mpya ya kuibua vivutio vilivyofichika vya Ziwa Nyasa.
“Hii barabara itatusaidia kusafirisha mazao yetu kwa haraka hadi bandarini, na hata kuyapeleka nje ya nchi,” anasema Mama Anna Mlagha, mkulima kutoka kijiji cha Ruanda.
Zaidi ya hayo, barabara hii inaunganisha Bandari ya Ndumbi na Bandari ya Mbambabay kiunganishi cha usafiri wa majini ambacho sasa kitapata nguvu mpya, na hivyo kuchochea shughuli za kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.