KAZI ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha Ndege Songea mkoani Ruvuma imefikia asilimia 97 na kiwanja hicho kinatarajia kukabidhiwa serikalini Januari 30 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi amesema serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Amesema mradi huo ulitekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya CHICCO toka nchini China kwa miezi 20 kuanzia Septemba 2019 hivyo unatarajiwa kukabidhiwa mwezi huu na ndege zinatarajiwa kuanza kutua usiku
Amezitaja kazi ambazo zimefanyika kuwa ni ukarabati na utanuzi wa njia ya kurukia ndege kutoka urefu wa meta 1625 na upana wa meta 30 hadi kufikia urefu wa meta 1740 na upana wa meta 30.
“Kazi nyingine zilizofanywa ni upanuzi wa maeneo ya usalama wa ndege,ukarabati na upanuzi wa eneo la maegesho ya ndege,ujenzi wa eneo jipya la maegesho ya ndege kwa dharura,jengo jipya la abiria na upakaji wa rangi wa alama za kiwanja’’,alisema Mhandisi Mlavi.
Amezitaja kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa mitaro,ujenzi wa uzio wa kuzunguka kiwanja,ujenzi wa barabara ya ndani ya kukagua usalama wa kiwanja,ufungaji wa taa za kuongozea ndege,ufungaji wa vifaa vya mawasiliano ya anga na ujenzi wa jengo la mitambo ya umeme.
Meneja huyo wa TANROADS Mkoa amezitaja kazi zilizoongezeka kuwa ni utanuzi wa njia ya kurukia ndege,ujenzi wa barabara ya nje ya kukagua usalama wa kiwanja,ujenzi wa jengo la muda la mitambo ya mawasiliano na anga na uongozi wa ndege.
Hata hivyo amesema utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia asilimia 97 na kwamba kazi zilizosalia ni mitambo ya umeme,mitambo ya kusukuma maji ,taa za kuongozea ndege na vifaa vya usambazaji mawasiliano ya anga ambapo amesema kazi zote zinatarajia kukamilika Januari 30,2023.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amemshukuru Rais kwa kutoa fedha za ukarabati wa kiwanja cha ndege na miradi mingine mikubwa ya kimkakati kukamilika mkoani Ruvuma.
Kanali Thomas amesema wananchi sasa wanahitaji kuona miradi yote inakamilika kwa asilimia 100 na kwamba wananchi wa Ruvuma wanatamani kuona sasa ndege zinatua usiku katika kiwanja cha Songea.
Ameyataja mahitaji ya abiria wanaotumia ndege katika Mkoa wa Ruvuma ni makubwa ambapo hivi sasa wanahitaji safari za usiku na mchana kwa kutumia ndege za ATCL.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema amesema Mkoa wa Ruvuma umepata uwanja wa kisasa wa ndege ambao utawezesha wasafiri kufika Songea mchana na usiku na kufanya biashara na kurejea Dar es salaam.
Amesema Mkoa wa Ruvuma una vivutio vya utalii na uwekezaji ambavyo sasa unaweza kuvifikia kwa haraka kwa kutumia usafiri wa anga.
Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege Songea Jordan Mchami amesema kabla serikali kuleta ndege za ATCL,wananchi wenye uwezo walisafiri kwa gharama kubwa Kwenda na kurudi Songea hadi Dar es salaam ilikuwa ni shilingi milioni moja.
Amesema hivi sasa kupitia ndege wa ATCL Kwenda na kurudi Songea hadi Dar es salaam ni kati ya shilingi laki tatu hadi nne kwa safari ya Kwenda na kurudi.
Amesema kiwanja cha Songea kina uwezo wa kutua ndege aina ya Bombadier yenye uwezo wa kubeba abiria 76 ambayo mara nyingi imekuwa inakuja na abiria 76 kwenda na abiria 76.
“Ndege inajaa hivyo tunatoa rai kwa kampuni nyingine za ndege kuanzisha safari na ATCL kuongeza safari za ndege ikiwezekana hata kila siku, tunatarajia kuanza safari za usiku taa zimeshafungwa tunasubiri kufanya majaribio ya kutua usiku ili hatimaye ndege zianze kutua usiku’’,alisema Mchami.
Uwanja wa ndege wa Songea ni miongoni mwa viwanja bora vya ndege Tanzania ambao ulijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Januari 10,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.