Na Albano Midelo PORI la Akiba la wanyamapori la Liparamba linapita katika wilaya za Songea,Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, limejaaliwa kuwa na vivutio ambavyo havipatikani katika hifadhi nyingine nchini. Liparamba ni hifadhi iliyopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambayo ina wanyama aina ya tembo ambao ni wakimbizi ikiwa na maana kwamba huwa wanavuka hadi hifadhi ya Niassa nchini jirani ya Msumbiji kisha kurudi Tanzania kupitia pori la Liparamba hadi Pori la Akiba la Selous. Pori hili pia limebarikiwa kuwa na wanyama adimu aina ya simba weupe ambao hawapatikani pori lingine lolote zaidi ya Liparamba hali ambayo inaweza kuvutia wageni wengi kutoka nje kutembelea katika hifadhi hii. Meneja wa Pori hilo Ramadhani Issomanga anasema pori la Akiba la Liparamba lipo katika ukanda wa wa misitu maarufu duniani ya miombo woodland inayokadiriwa kuwa na tembo zaidi ya 60,000 kulingana na utafiti ambao ulifanywa mwaka 2011 na Wizara ya Maliasili na Utalii. “Ni mara chache sana hapa duniani kuwepo kwa hifadhi moja ya wanyamapori ambayo inatumika na nchi mbili tofauti.Tanzania tuna bahati kwa kuwa kuna na hifadhi ya wanyamapori ya Liparamba inayotumiwa na wanyama upande wa Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji’’,issomanga. Anabainisha kuwa pori hilo lilikabidhiwa rasmi Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya usimamizi wa Idara ya Wanyamapori serikani Juni 5 mwaka 2006 ambapo pori hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 571 likiwa na eneo la kilometa za mraba 11,396. Anasema ukubwa wa misitu mizito minene iliyopo katika pori hilo inachangia kupunguza hewa ukaa(CO2) na kwamba pori hilo ni eneo muhimu katika mchakato wa (Carbon sink) ambao hupokea mvua za kutosha kwa msimu mmoja tu kwa mwaka. Issomanga anabainisha zaidi kuwa pori hilo lina mito mikubwa miwili ambayo ni mto Lunyere na mto Lumeme ambayo inamwaga maji yake katika mto Ruvuma ambao ni maarufu barani Afrika unaomwaga maji yake Bahari ya Hindi na kwamba pori lipo katika ukanda wa madini hivyo pori linaangaliwa dhidi ya uvamizi wa uchimbaji madini. “Miongoni mwa vivutio adimu ni uoto wa asili ya jamii ya miombo zikiwemo aina 60 za miombo,nyasi adimu aina 35,aina 80 za ndege na wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo tembo, simba, chui,parahali, tandala, pundamilia, nyati, kuro, pofu, kima, mamba,kiboko,ngiri na wanyama wengine’’,anasema Issomanga. Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo,pori hilo lina uoto wa asili ambao haujaharibiwa katika ukanda wa wilaya za Mbinga na Nyasa na kwamba pori hilo linatoa matunzo ya tembo wakimbizi kutoka Msumbiji na kuja Tanzania na kurudi Msumbiji na kwamba utafiti umebaini wanyama wengine wakifika Tanzania hawarudi Msumbiji. Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema kuwa pori hilo lina kiwango cha juu cha hifadhi ambacho kinatiliwa mkazo kisheria katika ulinzi, usimamizi,uendelezaji na matumizi ya malihai ikiwemo misitu,samaki na wanyamapori hivyo kuhifadhiwa kumejumuisha sekta nzima ya maendeleo ya mazingira,maliasili na utalii kwa gharama nafuu. "Hili eneo ni la kipekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo,lipo karibu na ziwa Nyasa,wengi watavutiwa na eneo hili kuona msitu mzuri wa asili usioharibiwa sanjari na wanyama adimu wakiwemo chui,simba,palahala na tandala wakubwa", anasema. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme anatoa rai kwa watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kwenda kutalii katika pori la akiba Liparamba lenye simba weupe na tembo wakimbizi hali ambayo inaongeza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii ambayo imeanza kufunguka katika Mkoa wa Ruvuma. Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetenga bajeti ya shilingi trilioni moja ili kupanua utalii katika ukanda wa kusini ikiwemo mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara. Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo ambaye ni Ofisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma |
|
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.