Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa na madaktari wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni muhimu katika jamii kwani zinatoa nafasi kwa wananchi kupata huduma stahiki.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan awamu ya pili uliofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
"Ni ukweli usiopingika huduma hii ni muhimu kwa jamii yetu hasa kwa vituo vinavyotoa huduma katika ngazi ya afya ya msingi, matarajio yangu ni kuwa uwepo wenu katika kambi hii utatoa nafasi kwa wananchi kupata huduma stahiki," alisema Kanali Ahmed.
Ameongeza kuwa wataalam hao wataifanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa, kwa kuwa Serikali imeboresha upatikanaji wa vifaa tiba na vituo vya kutolea huduma za afya vinaendelea kuboreshwa ikiwemo ujenzi na ukamilishwaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali za Halmashauri na Zahanati.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr. Louis Chomboko amebainisha kuwa madaktari hao watatoa huduma za kibingwa za magonjwa ya wanawake na ukunga, magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto na watoto wachanga, upasuaji na mfumo wa mkojo, mifupa na ajali pamoja na magonjwa ya kinywa na meno.
Dr. Chomboko amelitaja lengo la madaktari hao kufika mikoani ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuendeleza dhana ya kupata huduma bora.
Kwa upande wake Dr. Philip Steven Muhonji akizungumza kwa niaba ya madaktari bingwa amesema wao kama wahudumu wa afya wapo tayari kutoa huduma ili kutimiza adhma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesema zoezi hilo linaambatana na kuwajengea uwezo wataalam wengine katika maeneo ambayo bado hayajakamilika kwa kuwa huduma zitakapokuwa zinatolewa ndipo wataalam wengine wanajengewa uwezo.
Awamu ya kwanza ya huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za madaktari wa Dkt. Samia Suluhu Hassan zilitolewa kuanzia tarehe 6 hadi 10 Mei mwaka huu, na awamu hii ya pili huduma zinatolewa kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 3 mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.