MADAKTARI Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili,wanatarajia kuweka kambi ya siku tatu katika kituo cha afya cha Mtakanini kata ya Msindo wilayani Namtumbo,kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa Tezi Dume,Saratani ya matiti na mlango wa kizazi na Sukari.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vita Kawawa amesema ,huduma hizo zitatolewa kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Julai mwaka huu, na ni fursa nyingine kwa wananchi wa Namtumbo kufikiwa na huduma za matibabu za kibingwa katika kipindi cha mwezi mmoja.
“hii ni mara ya pili kupata timu ya Madaktari Bingwa kuja kutoa huduma katika Jimbo letu la Namtumbo,awali kufanyika zoezi la uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kutoka kwa timu ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI)”alisema Kawawa.
Amesema ,huduma hizo zitatolewa bure na kuwataka wananchi wa wilaya ya Namtumbo na wilaya nyingine katika mkoa wa Ruvuma,kuchangamkia fursa hiyo kwa kwenda kupata huduma za matibabu kutoka kwa Madaktari hao.
Amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kwenye kambi za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu zilizofanyika kwa muda wa siku saba katika Hospitali ya wilaya Namtumbo,kituo cha Afya Lusewa na Mputa.
Katika hatua nyingine Kawawa,ameipongeza serikaliya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutoa Sh.milioni 470 kati ya Sh.milioni 600 kwa ajili ya kujenga shule ya Sekondari Msisima kata ya Msisima wilayani Namtumbo.
Amesema ,shule hiyo imeleta nafuu kwa watoto wanaomaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya Sekondari ambao awali walitembea umbali wa kilometa 30 kwenda kata jirani ya Lusewa kufuata masomo na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kufika kidato cha nne.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.