Katika ukanda wa mikoa ya kusini mwa Tanzania, Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imegeuka kuwa kitovu cha mjadala mkubwa wa maendeleo ya madini.
Madini ya urani, mojawapo ya rasilimali muhimu kwa uzalishaji wa nishati ya nyuklia, yamegunduliwa kwa wingi katika eneo la Mto Mkuju. Hii si tu habari njema kwa wawekezaji bali pia kwa Tanzania, kwani mradi huu unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Tanzania: Nyumbani ya Utajiri wa Madini ya Urani
Tanzania imebarikiwa na hazina kubwa ya madini ya urani, jambo linaloifanya kuwa kivutio kwa wawekezaji wa kimataifa.
Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, mojawapo ya waendeshaji wakuu wa mradi wa urani Namtumbo, imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta hii. Serikali, kwa upande wake, imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia sera za madini na kodi zinazovutia wawekezaji.
Pamoja na utajiri wa rasilimali hii, Tanzania pia inanufaika na miundombinu bora inayowezesha usafirishaji wa madini haya. Bandari za Dar es Salaam na Mtwara ni lango muhimu la kusafirisha madini haya kwenda masoko ya kimataifa, huku vyuo vikuu na taasisi za mafunzo ya ufundi vikitoa wataalamu wa sekta ya madini.
Uwekezaji wa Mantra na Faida kwa Jamii
Majani Moremi Wambura, Meneja uendelevu wa kampuni ya Mantra Tanzania anasema Mantra Tanzania Limited haijawekeza tu katika uchimbaji wa urani bali pia katika jamii inayozunguka mgodi huo. Kupitia miradi ya kijamii, kampuni hii imeshirikiana na wakazi wa vijiji vya Mtonya, Likuyu Seka, na Likuyu Mandela ili kuboresha huduma za afya, elimu, na ajira. Mafunzo ya usalama kuhusu urani pia yametolewa kwa jamii ili kuhakikisha kuwa wanajua jinsi ya kujikinga dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza.
Athari za Mazingira na Hatua za Ulinzi
Madini ya urani yanahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha kuwa uchimbaji wake haudhuru mazingira. Mantra imechukua hatua za kuhakikisha kuwa maji yanayotumiwa kwenye uchakataji wa madini haya yanachakatwa upya na kurejeshwa katika mazingira kwa njia salama. Kampuni pia inafanyia tathmini mbinu mpya za uchimbaji rafiki wa mazingira ili kupunguza athari za shughuli zake.
Tanzania Katika Ramani ya Dunia ya Uranium
Mradi huu ambao unazinduliwa rasmi na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan unaanza kutekelezwa rasmi, hivyo Tanzania inakuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa madini ya uranium duniani.
Mradi wa madini ya Urani eneo la Mkuju unatarajiwa kutoa urani kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15, na Tanzania inaweza kuchangia hadi asilimia 4 ya uzalishaji wa urani duniani.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ana matumaini makubwa kwamba mradi huu utaiweka Tanzania katika nafasi ya juu katika sekta ya madini duniani.
Madini ya urani Namtumbo si tu fursa kwa wawekezaji, bali ni neema kwa uchumi wa Tanzania. Mradi huu unatoa nafasi za ajira, kuchochea ukuaji wa sekta nyingine, na kuinua viwango vya maisha kwa wakazi wa Namtumbo,Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.