Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mwl. Edith Mpinzile amewasisitiza walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati kushiriki kikamilifu katika mafunzo na kuyatumia vizuri ili yawe na manufaa kwa ustawi wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA kwa walimu wa Sekondari mkoani Ruvuma ambayo yanafanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea (Songea Girls) iliyopo Manispaa ya Songea.
Amewataka walimu kuthamini mchango wa Serikali katika mafunzo hayo na kuitumia fursa hiyo kujiandaa vizuri na masomo ya Sayansi ili mwaka huu Mkoa wa Ruvuma usisomeke katika orodha ya mikoa inayofanya vibaya kitaifa.
Naye Mratibu wa kituo cha mafunzo hayo Songea, Winchslaus Balige, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Mradi wa SEQUIP inaendelea kutoa mafunzo endelevu kwa walimu wa Fizikia, Baiolojia, Kemia na Hisabati pamoja na wathibiti ubora wa shule.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kufundisha masomo ya Sayansi na Hisabati kwa umahiri zaidi, kutumia mbinu bora za upimaji, na kutumia TEHAMA darasani, pia yanalenga kuwajengea uwezo wa kuandaa na kutumia zana mbalimbali na stadi za maabara, pamoja na kutumia vishikwambi kwa maandalizi ya ujifunzaji na ufundishaji.
Malengo mengine ni kuwajengea walimu uwezo wa kufanya tafiti tatuzi, kutatua changamoto za ufundishaji, na kuwajengea uwelewa juu ya sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na mtaala wa Elimu ulioboreshwa.
Pia, ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha umahiri wa walimu kutumia lugha ya Kiingereza katika kufundisha masomo ya Sayansi na kuimarisha uwezo wa wadhibiti ubora wa shule kufanya tathmini ya masomo hayo kwa mbinu shirikishi.
Dhima ya mafunzo hayo kwa walimu ni kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari nchini kwa kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu shirikishi, vifaa vya mtaala na zana za ufundishaji kulingana na mazingira yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.