MTAALAM kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dr. Justine Assenga amesema zaidi ya asilimia 60 ya magonjwa anayougua binadamu yanasababishwa na wanyama.
Dr.Assenga ameyasema hayo kwenye mafunzo ya utayari wa kukabili magonjwa ambukizi kwa timu za dharura za kukabili magonjwa kutoka mikoa hatarishi ya Ruvuma na Mtwara ambayo yanafanyika kwa siku tano kwenye ukumbi wa Hoteli ya Tiffany mjini Mtwara.
Kwa mujibu wa Mtaalam huyo kati ya asilimia hizo,asilimia 75 ya magonjwa hayo yanaambukizwa na wanyamapori na asilimia 20 kutoka wanyama wanaofugwa.
Ameyataja magonjwa sita hatarishi ya milipuko kuwa ni kimeta,kichaa mbwa,bonde la ufa,mafua makali ya ndege,kutupa mimba na ebola na amewataja baadhi ya wanyama ambao ni hatarishi katika kusambaza magonjwa hayo kuwa ni popo na panya.
Akifungua mafunzo hayo,Mkurugenzi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kanali Jimmy Matamwe ameitaja dhana ya afya moja kuwa inawakutanisha wataalam na wadau kutoka sekta mbalimbali hususani sekta ya afya,mazingira,maliasili,mifugo na wanahabari kutekeleza agenda ya usalama wa afya duniani.
“Dhana ya afya moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea vingi vinavyosababisha magonjwa ya binadamu,asilimia 60 vinatoka kwa wanyamapori na mifugo,maambukizi yanatokea pale binadamu anapoingilia masikani ya wanyama hao bila tahadhari”,alisema.
Hata hivyo amesema kwa nchi za Afrika hali ni hatarishi zaidi kwa kuzingatia kuwa bara hili hususani sehemu ambazo zinakaribia mapori makubwa ya wanyama ikiwemo Kongo Basin ni kitovu cha magonjwa ya milipuko kama vile ebola na homa ya bonde la ufa na hivi sasa ni virusi vya corona.
Kanali Matamwe amesema imedhirika kuwa ushirikiano wa watalaam katika mifumo ya afya moja hivi sasa ni agenda ya dunia nzima kwa sababu inapunguza gharama katika kushughulikia tishio la magonjwa yanayotokana na vimelea vyenye uwezo wa kutoka kwa wanyama kwenda binadamu.
Amesema Tanzania sio kisiwa hivyo kutokana na ongezeko la watu duniani,mabadiliko ya tabianchi na utandawazi umekuwa na mwingiliano mkubwa baina ya watu na wanyama katika mazingira yao na kusababisha kueneo kwa vimelea kwa haraka zaidi na kusababisha magonjwa kwa binadamu,wanyama na mimea.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) Niwael Mtui ameyataja malengo ya kutoa mafunzo kwa timu ya afya moja ni kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kuzuia na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kabla hayajatokea.
Mafunzo ya utayari wa kukabili magonjwa ambukizi ya mlipuko kwa timu za dharura yanafadhiliwa na FAO kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo yalianza kutolewa mwaka 2018.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 5,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.