MCHANGO wa Mkoa wa Ruvuma katika ukuaji wa uchumi wa Taifa umechomoza kwa kasi ya kuvutia, baada ya takwimu rasmi kuonyesha kuwa Pato la Taifa (GDP) katika mkoa huo limeongezeka kutoka Shilingi bilioni 2.37 mwaka 2012 hadi kufikia Shilingi bilioni 6.39 mwaka 2022 – ongezeko kubwa linalochagizwa na sekta ya madini na kilimo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mkoa wa Ruvuma umechangia wastani wa asilimia 10.5 ya Pato la Taifa kwa mfululizo wa miaka, hali inayoonesha kasi ya maendeleo na ongezeko la shughuli za kiuchumi katika kanda hiyo ya kusini mwa Tanzania.
Kwa upande wa sekta ya madini, makaa ya mawe ndiyo yanayoongoza katika kuimarisha uchumi wa mkoa huo. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, serikali ilifanikiwa kuuza tani 1,356,249.84 za makaa ya mawe kutoka Ruvuma, zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 144.9, kwa mujibu wa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Alphonce Bikulamchi.
Kupitia mauzo hayo, serikali imekusanya Dola milioni 3.9 kama mrabaha na Dola 914,034.68 kupitia ada za ukaguzi, kiasi kikubwa cha fedha ambazo zinasaidia kuimarisha mapato ya ndani. Madini hayo yaliuzwa ndani ya nchi, katika nchi jirani, barani Ulaya na Asia kupitia bandari za Mtwara na Dar es Salaam.
“Takwimu hizi ni kielelezo tosha kuwa sekta ya madini mkoani Ruvuma si tu injini ya maendeleo ya mkoa huu, bali pia ni nguzo muhimu ya ustawi wa Taifa,” alisema Mhandisi Bikulamchi.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2023, Ofisi ya Madini ya Mkoa huo tayari ilikuwa imekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 13, sawa na asilimia 64 ya lengo la mwaka ambalo ni Shilingi bilioni 41.
Uchimbaji wa makaa ya mawe ulianza rasmi mwaka 2011 na kampuni moja pekee – Tancoal Energy – lakini kufikia mwaka 2019, wawekezaji wengi walikuwa wamejitokeza, wakigeuza Ruvuma kuwa kitovu cha biashara ya makaa ya mawe nchini.
Mpaka sasa, ofisi ya Afisa Madini Mkazi Ruvuma imetoa jumla ya leseni 144 za utafutaji na uchimbaji wa madini, ikiwa ni pamoja na leseni za uchimbaji mkubwa, wa kati, na mdogo, pamoja na leseni za biashara kwa mawakala (dealers) na madalali (brokers).
Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/2025, serikali imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 105.1 kutoka sekta ya madini pekee mkoani Ruvuma, sawa na asilimia 126 ya lengo la makusanyo.
“Huu ni uthibitisho wa ufanisi katika usimamizi wa makusanyo ya fedha zinazotokana na shughuli za madini, ikichangiwa na ongezeko la mauzo ya madini,” alisema Mhandisi Bikulamchi kwa msisitizo.
Mkoa wa Ruvuma unazidi kujiimarisha kama nguzo ya uchumi wa Taifa, ukionesha jinsi rasilimali asilia zinavyoweza kuchochea maendeleo endapo zitasimamiwa kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.