Serikali kujenga barabara ya mchepuko
SERIKALI inatarajia kuanza kujenga barabara ya mchepuko kilometa 16 katika mji wa Songea ili kukabiliana na kero ya malori 1000 ya makaa ya mawe yanayopita mjini Songea kwa siku.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati anajibu ombi la wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea la kuomba kujengewa barabara itakayopita nje ya mji ili kuepuka kero ya malori ya makaa ya mawe.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwa barabara ya Songea hadi Makambako hivi sasa inabeba mizigo mingi na mizito hivyo serikali mwaka huu imeamua kuifanyia matengenezo makubwa kwa kuijenga upya ili iwe barabara ya kisasa.
“Mwaka huu tutaanza kujenga barabara ya lami kuanzia Lutukira sehemu ambayo imechoka sana hadi Songea mjini,ikiwa ni Pamoja na kujenga barabara ya mchapuko Songea mjini yenye urefu wa kilometa 16’’,alisema Naibu Waziri.
Amesema barabara hiyo ya mchepuko itasaidia magari makubwa kupita nje ya nchi badala ya kupita katikati ya mji na kwamba barabara za mchepuko zitapita sehemu tatu ambazo amezitaja kuwa ni eneo la Namanditi,Msamala na Sogea .
Amesema serikali imefanya tathmini ya fidia kwa wananchi wote waliopitiwa na barabara ya mchepuko ambapo tayari serikali imeandaa fedha za kuwalipa fidia zaidi ya shilingi bilioni nne ambazo zipo tayari hazina.
Hata hivyo amesema wakati ujenzi wa kipande hicho unaendelea serikali itaendelea kutafuta fedha za ujenzi wa kipande cha barabara ya kutoka Lutukira hadi Makambako.
Amesema licha ya serikali kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 37 za upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Songea,mwezi Septemba mwaka huu serikali italeta gari la kisasa za Zimamoto kwa ajili ya uwanja wa ndege wa Songea.
Mbunge wa Songea mjini na Waziri wa Sheria na Katiba Dkt.Damas Ndumbaro kwa niaba ya wananchi wa Songea ameishukuru serikali kwa kutenga bajeti katika mwaka huu wa fedha kujenga barabara ya mchepuko inayokwenda sanjari na ujenzi wa barabara mpya ya lami kutoka Songea hadi Lutukira kilometa 100.
“Kwa siku moja katika mji wa Songea malori 1000 yenye makaa ya mawe yanapita mjini Songea,barabara hii katikati ya mji wa Songea imekuwa kero na haiwezekani tena,tunaishukuru serikali kwa kutenga fedha mwaka huu ili kuanza ujenzi’’,alisema.
Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na wananchi wa Songea alipofanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma alisema amesafiri kwa njia ya barabara toka Dodoma hadi Songea na ameiona hiyo barabara ilivyochoka na kuchakaa hivyo serikali mwaka huu inaanza kujenga barabara hiyo kutoka Songea hadi Lutukira.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.