Ngoro ni aina ya kilimo kinachohifadhi mazingira kwa njia ya asili ambacho kinaaminika kilianza kutumika na wakulima wa kabila la wamatengo Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma zaidi ya miaka 300 iliyopita.
Kilimo cha ngoro kilianzishwa na wazee maarufu wa kabila la wamatengo waliotokea nchini Malawi katika karne ya 17 ambapo tayari vizazi zaidi ya 10 vimepita hivi sasa tangu kilimo cha ngoro kilipoanzishwa katika wilaya ya Mbinga.
Ngwatura Ndunguru Mbunge Mstaafu wa Mbinga anataja moja ya madhumuni ya kuanzisha kilimo hiki ni kuudhibiti udongo wa juu wa ardhi ambao kwa kawaida huondolewa na maji au upepo kutokana na mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba nyingi ya kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora.
Tunajua kuwa udongo ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi vizuri, Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya mmomonyoko ni hasara kubwa, kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno.
Njia za kuhifadhi ardhi zinaweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo kama ni maeneo ya mwinuko au tambarare.
Hata hivyo zinaweza kutumika njia mbili au tatu katika shamba moja.Ziko njia kuu mbili za kuhifadhi ardhi ambazo ni njia za asili au za kienyeji na njia ya kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina na wataalam.
Wataalam wakongwe kama akina Bike mwaka 1938, Stenhouse mwaka 1994, Temu na Bisanda mwaka 1966 wanaeleza kuwa Wamatengo walilazimika kutumia kilimo cha ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri uliopo katika miteremko hiyo.
Katika mashimo ya ngoro hupandwa mazao kama maharage, mahindi na ngano kwenye kingo za mashimo hayo. Mkulima hufyeka hufyeka shamba lake na kuzipanga nyasi zilizokatwa kwenye mashimo ya ngoro.
Mkulima akipindua udongo wa chini kuwa juu hukata nyasi na kwamba udongo wenye rutuba hugeuka kuwa mboji na rutuba huongezeka.Maji ya mvua yakisimama katika mashimo ya ngoro hulinda unyevu wa ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.
Inaaminika kuwa kilimo cha ngoro ambacho tunaweza kukiita draft agriculture kinahusishwa na shughuli za kuwepo kwa mapango ya kuishi.
Historia ya Wilaya ya Mbinga inaonesha kuwa, hapo zamani wananchi wa Wilaya ya Mbinga walikuwa na tabia ya kufanya kilimo cha kuhamahama.
Wakulima wakati huo walilima sehemu moja na wanapogundua sehemu hiyo rutuba imemalizika walikuwa wanahamia sehemu nyingine yenye rutuba na kuendesha kilimo bila kujali athari za kimazingira ambazo zilikuwa zinajitokeza kutokana na aina hiyo ya kilimo.
Kutokana na kuwepo kwa mapango, wazee hao wa kabila la wamatengo waliamua kuanzisha kilimo cha kulima na kufukia majani ili kupata mbolea ya asili hivyo kuendesha kilimo walichokiita ngoro katika sehemu moja bila kuhama huku wakirutubisha ardhi na kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokana na ardhi ya Mbinga kuwa na milima yenye miteremko mikali.
Historia inaonesha kuwa wamatengo tangu wameanza kutumia kilimo cha ngoro miaka 300 iliyopita hadi sasa wamekuwa wanazalisha vyakula kwa wingi na kuhifadhi mazingira kwa njia ya asili kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo kutokea kwenye miteremko ya milima ya umatengo wilayani humo.
Katika kilimo cha ngoro mvua zinaponyesha maji huingia kwenye mmea na majani yaliyowekwa chini yanaoza ambapo katika msimu mwingine majani yaliota kwenye shimo yatafyekwa,mazao yaliosalia yatavunwa na kutandazwa kwenye shimo na kufukuliwa majani ya mwaka jana ambayo tayari yanakuwa mboji.
John Mbunda (80) mkazi wa kijiji cha Kilanga Juu wilayani Mbinga anasema wamatengo walianzisha mfumo maalum wa kilimo cha ngoro uliyowasaidia uliyojulikana kwa kabila la wamatengo kwa jina la Ingoro.
Mfumo huo uliwawezesha kuendelea kulima kwenye maporomoko ya milima bila ya kusababisha mmomonyoko wa udongo au kuathiri vibaya rutuba kwenye mashamba yao.
Alex Ndunguru mkazi wa Kijiji cha Ilela anasema wenyeji wa Mbinga walilazimika kubuni kilimo cha ‘ngoro ili kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko ya Umatengo na kwamba ngoro ndiyo mkombozi katika kilimo kwa kuwa kilimo kimekuwa endelevu badala ya mfumo wa zamani ambao wamatengo walifanya kilimo cha kuhamahama.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.