MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga amezitaja njia sita ambazo zinaweza kuzuia kupata maambukizi ya Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona (UVIKO19).
Akizungumza wakati anatolea elimu ya UVIKO 19 kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa Songea Klabu mjini Songea,Dr.Kanga amezitaja njia hizo kuwa ni kuvaa vema barakoa na kuwa mbali na jirani yako.
Njia nyingine amezitaja kuwa ni kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,kutumia vipukusa mikono,kufanya mazoezi,kupata lishe bora na kupata chanjo ya UVIKO 19 .
Hata hivyo amesema katika njia zote sita,kupata chanjo ya UVIKO 19 imebainika kisayansi kuwa ndiyo kinga ya uhakika zaidi ukilinganisha na njia nyingine.
“UVIKO 19 haina tiba kama ilivyo kwa UKIMWI au magonjwa yoyote yanayosababishwa na kirusi,kinachoweza kutibiwa ni dalili za ugonjwa,dawa pekee ya kukabiliana na UVIKO 19 kujikinga kwa kutumia chanjo’’,alisisitiza
Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akipata chanjo ya UVIKO 19
Amezitaja faida za chanjo ya UVIKO 19 kuwa ni kutengeneza kinga ya mwili ambayo ina uwezo mkubwa wa kumkinga mtu anapopata ugonjwa hawezi kufikia hatua mbaya ukilinganisha na mtu asiyepata chanjo na kwamba chanjo ya UVIKO 19 inazuia vifo na mtu kuwa mahututi..
Amesema utafiti ambao umefanyika nchini Afrika ya Kusini umebaini kuwa asilimia 96 ya wagonjwa na vifo vilivyotokea nchini humo ni kutoka kwa watu ambao hajawapata chanjo ya UVIKO hivyo kuna kila sababu ya watanzania kujitokeza kwa hiari kuchanja chanjo hiyo kuzuia vifo na kuzidiwa na ugonjwa.
Ametahadharisha tangu kutengenezwa kwa chanjo ya UVIKO hadi kuharibika huchukua miezi sita ambapo hadi sasa katika Mkoa wa Ruvuma watu 3100 wamejitokeza kwa hiari kupata chanjo hiyo kati ya chanjo 30,000 zilizotolewa katika Mkoa sawa na asilimia 10.
Hata hivyo amesema takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa Mkoa wa Lindi unaongoza kwa kufanya vizuri katika utoaji chanjo ambapo asilimia 34 ya wakazi wa Mkoa huo wamepata chanjo.
Amesema ili watanzania wapate kingakundi inatakiwa asilimia kati ya 60 na 70 kujitokeza kupata chanjo kwa hiari.
Dr.Kanga ameitaja Sayansi sio imani na wala haibahatishi badala yake inakwenda na utafiti ambapo amesisitiza kuwa hakuna dawa wala chanjo ambayo inazuia kwa asilimia 100.
Mganga Mkuu huyo amesisitiza kuwa mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 anaweza kupata chanjo ya UVIKO 19 na amewataja wasiostahili kupata chanjo hiyo kuwa ni akinamama wajawazito na wanaonyonyesha watoto chini ya miezi sita.
Pichani Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga akipata chanjo ya UVIKO 19
Amezitaja dalili za UVIKO 19 kuwa ni homa ndani ya siku 14,kukoa,mafua,kuchwa kuuma,mwili kuchoka na kwamba wimbi la tatu la UVIKO 19 halina dalili maalum hivyo unapojisikia nenda kupima ili tatizo lifahamike mapema ambapo amezitaja nchi zinazoongoza kwa maambukizi hivi sasa ni India na Msumbiji.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki ametoa rai kwa wataalam wa afya kuwa na mlipuko wa kutoa taarifa sahihi za chanjo ya UVIKO 19 ili kukabiliana na wapotoshaji wanaotumia mitandao kuchanganya wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 24,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.