HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa Januari 24 kwa kupanda miche ya miti 6200 katika chanzo cha maji Namanditi kinachopeleka maji yake katika Mto Ruvuma.
Wananchi wa Kata ya Ruhuwiko wakiongozwa na madiwani wa Manispaa ya Songea walishiriki kupanda miche ya miti ya asili.Mgeni rasmi katika zoezi hilo alikuwa ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji.
Awali akitoa taarifa ya Idara ya Maliasili Katika Manispaa ya Songea,Mkuu wa Idara hiyo Godfrey Luhimbo alizitaja shughuli za kibinadamu kuwa ndiyo chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira ambapo katika Manispaa ya Songea uharibifu aliutaja kuwa unatokana na uvamizi wa misitu ya hifadhi.
Sababu nyingine alizitaja kuwa ni ukataji miti hovyo kwenye vyanzo vya maji na kwenye misitu ya hifadhi kwa lengo la kuzalisha mazao ya misitu kama vile mkaa,nguzo,kuni na mbao na uwindaji wa wanyama
“Kutokana na uharibifu wa mazingira tunakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kuongezeka kwa joto la dunia,unyeshaji wa mvua usiokuwa na mpangilio,ukame na maradhi mbalimbali yanayomkabili binadamu’’,alisisitiza.
Katika kukabilina na changamoto hizo ameitaja mikakati inayofanywa na Idara ya Maliasili kuwa ni kutoa elimu,kupanda miti kila mwaka katika maeneo mbalimbali na kufanya doria za mara kwa mara ili kudhibiti uharibifu wa misitu.
Mgeni rasmi Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea akizungumza mara baada ya kushiriki zoezi la upandaji wa miti hiyo,ametoa rai kwa wakazi wa Songea na watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanavilinda vyanzo vyote vya maji vilivyopo na kupanda miche ya miti katika vyanzo ili viwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 25,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.