Watumishi 12 wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wamezeshwa pikipiki ikiwa ni jitihada za Halmashauri hiyo katika kutatua changamoto ya usafiri na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye ambaye alikua Mgeni Rasmi kwenye hafla ya ugawaji wa pikipiki hizo iliyofanyika Aprili 19, 2021 Shule ya Sekondari Kigonsera amempongeza Mkurugenzi na uongozi wa Halmashauri kwa kununua pikipiki hizo na kuomba mpango huo kuwa endelevu ili watumishi wote waliokusudiwa waweze kupata uwezeshwaji huo huku akiwaasa walionufaika na mgao huo wa pikipiki kuzingatia matumizi sahihi na yaliyokusudiwa.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Mbinga kukabidhi pikipiki hizo kwa walengwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Juma Mnwele amesema pikipiki hizo zenye thamani ya shilingi milioni 28 zimenunuliwa ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Halmashauri hiyo katika kutatua na kuondoa tatizo la usafiri na kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi na kuahidi uendelevu wa mpango huo wa kuwezesha watumishi.
Bw.Mnwele ametoa rai kwa wote walionufaika na awamu hii kwa kuwakumbusha kuwa pikipiki hizo ni mali ya serikali, hivyo wanapaswa kuzingatia matumizi sahihi na yaliyokusudiwa na kuwasisitiza kujiepusha na ulevi kila mara wanapoendesha vyombo hivyo vya moto.
“Kama tunavyofahamu pikipiki haina urafiki na mlevi, na kama ambavyo watu husema ukinywa bia moja na pikipiki nayo hunywa bia moja; vilevile unapokunywa bia nne pikipiki nayo inakunywa bia nne. Maana yangu ni kuwa msiendeshe pikipiki mkiwa mmelewa”. Amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Mhe. Desderius Haule amesema pikipiki hizo zimenunuliwa ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya vikao juu ya kutenga fedha na kuhakikisha wanatatua kero ya usafiri kwa watumishi wa Halmashauri hiyo na kuongeza kuwa hategemei matukio ya upotevu wala uharibifu wowote yatakayosababishwa na uzembe na wao kama madiwani watasimamia kikamilifu kwenye maeneo yao.
“Kwa kuwa ni fedha za Halmashauri tutakapoona aliyekabidhiwa hajali usalama wa chombo hatutasita kubadilisha matumizi; tunaweza tukanunua baiskeli tukakupa badala yake ambayo pengine ndio utakua na uwezo wa kuitunza. Sina maana kwamba mnyang’anywe, ninachosisitiza pikipiki hizi ziwe ni kwa ajili ya utendaji kazi na ziwasadie kuwahudumia wananchi”. Amesema mwenyekiti huo.
Orodha na mchanganuo wa watumishi waliopata pikipiki kwenye awamu hii ya kwanza ni Maafisa Kilimo wa Kata 6 za Langiro, Linda, Amani Makolo, Mbuji, Namswea na Matiri, Watendaji wa Kata 4 za Matiri, Kigonsera, Kipapa na Muungano. Wengine ni Maafisa Mifugo wa Kata 2 za Mkumbi na Mikalanga.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imekua na utaratibu wa mara kwa mara wa kuwezesha watumishi wake kwa namna na njia mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa sera na mpango wa Halmashauri hiyo ya kuwezesha watumishi wake. Ikumbukwe ndani ya mwaka huu wa fedha 2020/2021 mnano mwezi Disemba jumla ya walimu 105 walioajiriwa na kupangiwa kufanya kazi kwenye shule za msingi na sekondari ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga waliwezeshwa na Halmashauri hiyo kwa kupatiwa magodoro na majiko ya gesi yenye thamani ya shilingi milioni 27.3
Imeandikwa na:
Salum Said
Afisa Habari
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.