SERIKALI imetoa kiasi cha Sh.milioni 900 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya majengo katika Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando,wakati akitoa taarifa ya ujenzi na ukarabatiu huo kwa Waandishi wa Habari walioko kwenye ziara maalum ya kutembelea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
Alisema,kiasi hicho cha fedha kitatumika kujenga majengo matatu ambayo ni jengo la upasuaji,jengo la wagonjwa wa nje(OPD) na ukarabati wa jengo la maabara ambayo yakikamilika yatawezesha wananchi wanaofika katika Hospitali hiyo kupata huduma bora.
Marando alisema,fedha hizo zinakwenda kuimarisha utendaji kazi kwa watumishi wa sekta ya afya na kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali ya wilaya.
Aidha alisema,katika kipindi cha miaka miwili Rais Dkt Samia ameipatia wilaya ya Tunduru zaidi ya Sh.bilioni 231 kati ya hizo Sh.bilioni 33.9 zimekwenda kwa Halmashauri ya wilaya ili kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa Marando,fedha nyingine zimepelekwa kutekeleza miradi ya Serikali kuu ikiwemo ya maji inayotekelezwa na kusimamiwa na wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)nishati ya umeme vijijini(Rea) na Tanesco.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha hizo,kwani ni jambo la ajabu na kushukuru kwa wilaya hiyo kupata fedha nyingi katika kipindi cha miaka miwili tangu ilipoanzishwa mwaka 1905.
Katika hatua nyingine Marando alisema,wamepokea jumla ya Sh.milioni 300 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa dharura,hata hivyo kutokana na mapungufu yaliyojitokea wakati wa ujenzi Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ililazimika kuongeza Sh.milioni 69.
Alisema kuwa, kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na watumishi watakaofanya kazi katika jengo hilo wamepata mafunzo ya namna ya kutoa huduma na matumizi ya vifaa vilivyofungwa.
Amewapongeza wananchi wa wilaya ya Tunduru, kukubali kutoa ardhi yao bure na kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa miradi hiyo muhimu ambayo inakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na Taifa na kutunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo yao.
Kwa upande wake kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Wilson Mping’wa alisema,mradi huo ni kwa ajili ya wagonjwa wote wa dharura wa wilaya ya Tunduru maeneo mengine hapa nchini watakaohitaji kupata hudumaza dharura.
Alisema,jengo hilo litasaidia sana kupunguza vifo vilivyokuwa vinatokea kwa sababu ya kukosa huduma za dharura katika wilaya ya Tunduru na kupunguza gharama za rufaa ya kupeleka wagonjwa hadi Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma (HOMSO) iliyopo umbali wa kilomita 265.
Alisema,ndani ya jengo hilo kumefungwa vifaa mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa kupumua na matarajio ni kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.
Mkazi wa kijiji cha Muhuwesi wilayani humo Metus Lwiza,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kujenga jengo hilo ambalo litawasaidia wananchi kupata huduma muhimu na za haraka wakiwemo wajawazito na wanaopata ajali za pikipiki na magari.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.