Na Albano Midelo
Ukiwa pembezoni mwa Mto Ruvuma, ambao pia ni mpaka wa asili kati ya Tanzania na Msumbiji, unasimama kwa fahari Msitu wa Hifadhi ya Taifa wa Mazingira Asilia Mwambesi ni hazina iliyofichwa ya viumbe hai, historia, na vivutio vya kipekee vya asili.
Msitu huu mkubwa wenye zaidi ya hekta 112,000 uliopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, ulianzishwa mwaka 1956, na kupandishwa hadhi kuwa msitu wa taifa katika mwaka 2017/2018. Kupandishwa hadhi huku kunalenga kulinda bioanuwai tajiri inayopatikana hapa, inayojumuisha mamia ya spishi za wanyama, ndege, na mimea adimu duniani.
Viumbe Adimu na wa Kipekee
Meneja wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Tunduru, Denis Mwangama, anasema Mwambesi si tu kimbilio la wanyamapori kama simba, tembo, swala, nyati, nyani na chui, bali pia ni makazi ya ndege wa kipekee duniani anayeitwa Pentiole.
Utafiti wa mwaka 2015 uliofanywa na PALMS Foundation umebaini kuwa ndege huyu mdogo mzuri alihamia kutoka Madagaska baada ya makazi yake kuharibiwa na shughuli za binadamu.
Ndege huyu husifika kwa tabia ya kipekee – huogelea kwenye mawimbi ya maporomoko ya maji, akisaka samaki hai ambao ndio mlo wake pekee. Anaonekana zaidi kwenye Maporomoko ya Sunda, yaliyoko ndani ya hifadhi, sehemu ambayo pia ni kivutio kikubwa cha watalii.
“Tanzania tuna bahati kuwa na ndege wa pekee duniani, Pentiole, ambaye anaishi ukingoni mwa maporomoko ya Sunda Waterfalls,” anasisitiza Mwangama.
Historia Iliyofichwa Ndani ya Mapango
Maporomoko ya Sunda si kivutio cha sasa pekee, bali pia ni eneo lenye historia nzito ya vita ya Majimaji (1905–1907).
Mwangama anasema mapango yaliyo juu ya maporomoko hayo yalitumika na wapiganaji kujificha wakati wa vita, na Mto Ruvuma ulikuwa tegemeo kubwa la maji kwa wapiganaji chini ya uongozi wa Kinjeketile Ngwale.
Aidha, kuna ushahidi kuwa Mto Ruvuma ulikuwa njia kuu ya biashara ya meno ya tembo na watumwa iliyotumiwa na Wajerumani na Waarabu waliovuka kutoka Msumbiji. Eneo hili linaonekana kuwa makutano ya historia, urithi wa asili, na maisha ya kisasa ya uhifadhi.
Mazingira Yanayovutia Utalii wa Kiikolojia
Deborah Mwakanosya, mwakilishi wa Meneja wa Msitu huo, anasema Mwambesi ni msitu wa pili kwa ukubwa nchini baada ya Kilombero. Ukiwa umezungukwa na Mto Ruvuma, msitu huu unasheheni mimea adimu kama mipozipozi, miti yenye tabia ya kipekee ya kudondosha maji kutoka kwenye matawi yake, aina ambayo inapatikana katika maeneo machache duniani.
Msitu huu pia ni makazi ya wanyama wa mtoni kama mamba na viboko, ambao huonekana kwa wingi hasa wakati wa masika, wakivutia wageni wanaofika kutalii.
Watalii wanaopenda matukio wanaweza kufurahia utalii wa kuteleza kwa mitumbwi kwenye Mto Ruvuma, huku wakishuhudia mandhari murua ya fukwe za asili zilizo kando ya mto.
Kutoka Kambi ya Uwindaji hadi Kituo cha Uhifadhi
Kabla ya kutangazwa kuwa hifadhi, Mwambesi ulikuwa na vitalu vya uwindaji wa kitalii vilivyokuwa chini ya Kampuni ya Tandara Hunting Safaris, iliyokuwa na kambi maarufu ya wawindaji iitwayo Big Game. Lakini sasa, matarajio mapya yamechipua – uhifadhi wa mazingira na ukuzaji wa utalii endelevu.
“Msitu huu ni hazina ya taifa. Tuna kila sababu ya kuutangaza na kuulinda, kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo,” anahitimisha Mwangama.
Msitu wa Mwambesi si tu mapafu ya Kusini mwa Tanzania bali ni urithi hai unaoelezea hadithi ya asili, mapambano, na matumaini mapya.
Katika ulimwengu unaopoteza kasi ya uhusiano wa binadamu na mazingira, Mwambesi unasimama kama kielelezo cha matumaini na mfano bora wa uhifadhi unaozingatia historia, tamaduni, na maisha ya sasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.