WAKULIMA wa zao la ufuta katika Wilaya za Namtumbo,Songea na Tunduru mkoani Ruvuma wameanza kunufaika na zao hilo baada ya kupokea shilingi bilioni 16.8 tangu kuanza kuuza zao hilo kwa mfumo wa stakabadhi ghalani Apirili 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme wakati anafungua kikao maalum Baraza la madiwani la Halmashauri ya Namtumbo cha kujadili Hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Mpaka sasa katika minada ya Songea,Namtumbo na Tunduru zimeuzwa kilo milioni 8.2 za zao la ufuta zilizosababisha wakulima kupata sh.bilioni 16.8 ambazo zitaendelea kuongezeka kupitia minada inayokuja’’,alisisitiza Mndeme.
Mndeme amesema tangu kufunguliwa kwa mnada, vyama vya ushirika AMCOS kupitia zao la ufuta vimekwishapata zaidi ya sh.milioni 500 na ushuru uliopatikana kwenye vyama vikuu vya ushirika SUNAMCO na TAMCO ni shilingi milioni 2.48.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuonesha mafanikio makubwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kwamba mfumo huo utaendelea kutumika kwenye mazao ya soya na Mbaazi ili kulinda haki ya wakulima.
Mndeme amesema Mkoa wa Ruvuma msimu huu unatarajia kuendelea kuwa gwiji katika mazao ya chakula ambapo mahitaji ya chakula katika Mkoa wa Ruvuma ni tani laki 3.38 hadi sasa Mkoa una ziada ya chakula zaidi ya tani laki tisa.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini na kwamba hadi kufikia Mei 15 mwaka huu zilikuwa zimevuna tani milioni 1.3.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.