Mkoa wa Ruvuma unazidi kupiga hatua katika kuboresha sekta ya afya, ambapo Kwa jumla, mkoa una vituo 473 vya kutoa huduma za afya, vinavyojumuisha hospitali, vituo vya afya, na zahanati zinazosimamiwa na Serikali, Mashirika ya Dini, na sekta binafsi.
Muundo wa Vituo vya Afya
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko anasema Ruvuma una hospitali 18, ambapo hospitali tisa zinamilikiwa na Serikali, saba ni za Mashirika ya Dini, huku hospitali mbili zikimilikiwa na watu binafsi.
Mkoa una vituo vya afya 50, ambapo asilimia kubwa ikiwa ni vituo vya afya 39 vinamilikiwa na Serikali, huku 11 vikiwa chini ya Mashirika ya Dini na sekta binafsi.
Kwa upande wa zahanati, mkoa una jumla ya 341, kati ya hizo 277 zinamilikiwa na Serikali na 64 zinamilikiwa na sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Dini. Muundo huu wa vituo vya afya unalenga kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wananchi wa maeneo yote ya mkoa.
Changamoto ya Upatikanaji wa Rasilimali Watu
Pamoja na uwepo wa vituo vingi vya afya, upungufu wa watumishi wa afya ni moja ya changamoto kubwa inayoukabili mkoa. Kwa sasa, kuna watumishi wa afya 3,323, sawa na asilimia 47.2 ya mahitaji halisi ya watumishi 7,043.
Ongezeko la vituo vipya vya huduma limechangia kupungua kwa uwiano wa watumishi waliopo katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma. Hali hii inasababisha msongamano kwa watumishi waliopo na kupunguza ufanisi wa utoaji huduma za afya kwa wananchi.
Matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Serikali (GoTHOMIS)
Katika jitihada za kuimarisha utoaji wa huduma za afya, Serikali imeanzisha matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa GoTHOMIS kwa lengo la kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Hadi kufikia Desemba 2024, jumla ya vituo 307 kati ya 325 vya serikali vilikuwa vimesimikwa mfumo huu, ikiwa ni asilimia 94.5.
Mkoa wa Ruvuma umeonesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake. Uwepo wa vituo vingi vya afya, pamoja na jitihada za kuboresha mifumo ya kielektroniki, ni hatua muhimu katika safari ya kuimarisha sekta ya afya mkoani hapa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.