Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana anasema taarifa za tafiti za awali za makaa ya mawe katika maeneo ya Mbalawala Mbinga ni tani milioni 99.5, Mbuyula Mbinga tani milioni 15.1 na Muhukuru Songea tani milioni 27.
Kwa mujibu wa Nkana tafiti katika eneo la Njuga wilaya ya Songea tani milioni 23, Mbambabay katika kijiji cha Malini kata ya Mtipwili tani milioni 29, kijiji cha Liweta Kata ya Mbaha Nyasa tani milioni 34 na kwamba ubora wa makaa ya mawe yanayopatikana kwenye maeneo hayo yana wastani wa Calorific Value (CV)5,000 hadi 7,000.
Hata hivyo Afisa Madini Mkazi huyo wa Mkoa wa Ruvuma anasema uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe unafanyika katika maeneo ya Mbalawala,Mbuyula, Mbambabay, Muhukulu na Liweta.
Anawataja wateja wakubwa wa makaa ya mawe yanayochimbwa katika maeneo hayo kwa sasa kuwa wapo ndani ya nchi na katika nchi jirani za Rwanda, Kenya na Uganda.
“Makaa ya mawe yanayozalishwa na kuuzwa kwenye masoko hayo ni kiasi cha wastani wa tani 55,000 kwa mwezi ambapo kati ya kiwango hicho asilimia 70 yanauzwa ndani ya nchi’’,anasema Nkana.
Anaitaja hazina ya makaa ya mawe iliyopo kwenye maeneo hayo yote inakadiriwa kuwa ni ziadi ya Tani milioni 227.6 ambapo uzalishaji unaofanyika kwa sasa ni wa wastani wa tani 55,000 na kwamba Inakadiriwa makaa hayo yatachimbwa kwa miaka zaidi ya 300.
Mataifa mengine yaliyoonesha nia ya kununua makaa ya mawe ya mkoa wa Ruvuma ni India na China. Licha ya makaa ya mawe ya Ngaka na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuuzwa na kutumika viwandani ni muhimu kutumia makaa ya mawe kuzalishia umeme.
Mhandisi Nkana anabainisha kuwa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe gharama zake ni nafuu kwa wananchi na pia umeme huo utachochea ukuaji wa viwanda nchini hasa katika awamu ya tano ambayo inasisitiza serikali ya viwanda.
Utafiti umebaini kuwa umeme unaotokana na madini ya makaa ya mawe ndio unaotegemewa zaidi na mataifa mengi yaliyoendelea duniani.Takwimu zinaonesha kuwa makaa ya mawe yanachangia asilimia 41 ya umeme unaozalishwa duniani,umeme wa maji asilimia 16,umeme wa gesi asilia asilimia 20, nyukilia asilimia 15 na umeme wa mafuta kwa kutumia jenereta ni asilimia sita tu.
Miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani ni yale ambayo yanatumia umeme wa makaa ya mawe.Mataifa hayo ni Afrika Kusini inayotumia asilimia 93 ya umeme wa makaa ya mawe,Poland asilimia 92 na China asilimia 79.Nchi nyingine ni Australia asilimia 77, Kazakhstan asilimia 70, India asilimia 69, Israel asilimia 63, Jamhuri ya Czech asilimia 60, Morocco asilimia 55,Ugiriki asilimia 52,Marekani asilimia 49 na Ujerumani asilimia 46.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.