MKOA wa Ruvuma umeongoza kitaifa zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 91 kwa kutoa chanjo kwa watu 44,549 sawa na asilimia 148.5.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati anafungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza wanaruvuma kwa mwitikio mkubwa ambao kwa hakika umesababisha Mkoa wetu umeongoza kitaifa’’,alisema Brigedia Jenerali Ibuge.
Amesema Mkoa wa Ruvuma ulianza rasmi utekelezaji wa chanjo kwa wananchi Septemba 22 hadi Oktoba 14 mwaka huu,ambapo Mkoa ulivuka malengo kwa kumaliza dozi 30,000 ulizopewa kwa awamu ya kwanza na kuongeza dozi nyingine ziada 14,000 hivyo kufikia dozi zaidi ya 44,000.
Hata hivyo amesema tayari serikali ya Tanzania imepokea dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya UVIKO 19 aina ya sinopharm kwa ajili ya kuendelea kuwapatia wananchi wake chanjo ambapo Mkoa wa Ruvuma umeletewa dozi zaidi ya 31,000 ambazo zinatarajiwa kuanza kutolewa kwa wananchi Oktoba 25 mwaka huu.
Amewaagiza watendaji wa Halmashauri zote mkoani Ruvuma kuhakikisha wanasambaza chanjo haraka katika vituo vyote 298 vinavyotoa chanjo na kwamba wataalam wa afya watoe elimu ya chanjo ya sinopharm ili ifahamike vizuri kwa wananchi kabla ya kuamua kuchanja kwa hiari.
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Ruvuma Winbroad Mvile ameitaja chanjo ya sinopharm kuwa inatolewa mara mbili ili kukamilisha dozi na kwamba chanjo hiyo inatengeneza kinga dhidi ya UVIKO 19 kwa asilimia 95.
Akizungumzia mgawanyo wa chanjo hiyo kwa kila Halmashauri mkoani Ruvuma,Mratibu huyo amesema Mkoa umeletewa dozi zaidi ya 31,291 za sinopharm ambapo Manispaa ya Songea imepewa dozi 5300,Tunduru 5300,Namtumbo 5300, Halmashauri ya Mbinga 3572,Nyasa 3572, Halmashauri ya Songea 3572,Mbinga Mji 3572 na Madaba 1103.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga ametoa rai wananchi ambao hawakupata chanjo katika awamu ya kwanza kujitokeza ili Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kufikia hatua ya kupata kinga kundi (Herd Immunity) ili kufikia asilimia 60 hadi 70 ya watu wawe wamepata chanjo.
Akizungumzia chanjo ya sinopharm,Dr.Kanga amewataja walengwa wa chanjo hiyo kuwa ni mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kwamba chanjo hii pia inatolewa kwa akinamama wajawazito na wanaonyonyesha.
Hata hivyo amesema mtu yeyote ambaye hajachanja chanjo ya kwanza ya Jassen& Jassen anaruhusiwa kupata chanjo ya pili ya sinopharm na kwamba chanzo zote ni salama na zina uwezo wa kujikinga na UVIKO 19 kwa asilimia 95.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 22,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.