MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Wilbert Ibuge ambae amewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Mh Pololet Mgema amezindua Bodi ya PAROLE Mkoani Ruvuma.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea.
Akizungumza kabla ya Uzinduzi huo amempongeza Mwenyekiti wa Bodi hiyo pamoja na wajumbe wote kwa kuteuliwa katika nafasi hii ya muhimu.
Hata hivyo Mgema amesema kuteuliwa kwao kuwa wajumbe wa Bodi kumetokana na kukidhi vigezo pamoja na uwezo wao ambao utasaidia Bodi ya Mkoa wa Ruvuma kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa ufanisi mkubwa.
‘’Ndugu wajumbe majukumu ya Bodi ya PAROLE kama ilivoainishwa katika sheria ni kama ifuatavyo kupitia na kujadili majalada ya wafungwa waliopendekezwa kunufaika na mpango, pia kutoa mapendekezo kwa wafungwa waliokidhi vigezo vya kunufaika na mpango pamoja na kuwasilisha mapendekezo ya majalada ya wafungwa waliopendekezwa kunufaika na mpango wa PAROLE’’ amesema Mgema.
Kwa upande wake Katibu wa Bodi ya PAROLE ambaye ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi wa Magereza Willington Willbard amewataja wajumbe wa Bodi ya PAROLE jumla wapo 11 kati yao wajumbe watano wameteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na wajumbe sita wameainishwa na Sheria ya PAROLE ya iliyopitishwa na Bunge ya 1994.
Naye Mjumbe wa Bodi ya PAROLE akizungumza kwa niaba ya wajumbe wake Vestina Nguruse ametoa shukurani kwa Mgeni rasmi kwa maneno mazuri, maelekezo ya miongozo na ufafanuzi wa mambo ya msingi pia wamehaidi kutekeleza jukumu hili kwa uaminifu na uzalendo.
PAROLE ni utaratibu wa wafungwa kutumikia kifungo nje ya gereza kabla ya kumaliza kutumikia vifungo vyao baada ya kukidhi sifa na vigezo vilivoainishwa katika Sheria ya PAROLE.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Ofisi ya Habari ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Machi 3 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.