WANANCHI wa kijiji cha Amanimakolo Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wametakiwa kutunza na kulinda miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kumaliza kero ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa j na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, mara baada ya kuzindua rasmi mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi ya mazingira(Ruwasa)wilaya ya Mbinga.
Alisema,Serikali kupitia Ruwasa inatekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali,hivyo ni jukumu la wananchi kuhakikisha wanalinda na kutunza miradi hiyo pamoja na vyanzo vya maji vilivyopo kwa manufaa yao.
Rc Laban alisema,wadau wakubwa na muhimu wenye wajibu wa kulinda miradi hiyo ni watumiaji wenyewe,kwa kuwa hata inapotokea changamoto ya huduma ya maji waathirika wakubwa ni wananchi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa,utunzaji wa mradi huo na chanzo chake cha maji ni jambo muhimu ambalo linawahusisha wadau na wananchi wanaoishi katika kijiji hicho na maeneo ya jirani ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wa serikali ya kijiji na kata kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu watakao hujumu mradi huo.
Alisema,Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan ina dhamira ya kweli ya kumtua mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2025,hivyo amewaasa wananchi kulinda mradi huo kwa gharama yoyote.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga,ameishukuru serikali kutekeleza mradi huo kwani utasaidia sana kumaliza kero ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2020 na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa).
Alisema,mradi ulikuwa unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani kwa fedha za mfuko wa maji ambapo jumla ya Sh.milioni 82,514,784.95 zililetwa na kutumika na hadi kufikia mwezi Disemba 2021 mradi ulitekelezwa kwa asilimia 30.
Aidha alieleza kuwa,mwezi Februari mwaka 2022 mradi ulianza kutekelezwa tena na mkandarasi kwa kutumia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 kwa gharama ya Sh.milioni 448,57,207.00.
Alisema katika utekelezaji huo, Ruwasa imenunua mabomba yenye thamani ya Sh.milioni 243,120,962 na hivyo kufanya gharama halisi za mradi huo kufikia Sh.milioni 774,214,953.55.
Aliongeza kuwa,mradi umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutoa huduma na uko kwenye kipindi cha maangalizi ya miezi 12 hadi Juni 2023 utakapokabidhiwa rasmi.
Sinkala alisema kuwa, hadi sasa mkandarasi ameshalipwa Sh.363,931,977.40 kati ya Sh.448,579,207.00 zilizopo kwenye mkataba na fedha zilizobaki atalipwa baada ya kukamilisha mapungufu mbalimbali anayotakiwa kuyafanyia kazi.Alisema,mradi huo utawanufaisha wakazi 5,022 wa vijiji viwili vya Amanimakolo na kijiji cha Mkeke vilivyopo kata ya Amanimakolo pamoja na wakazi wa kitongoji cha Mkeso kilichopo katika kijiji jirani cha Luhagara.
Alisema,awali kijiji cha Amanimakolo hakikuwa na huduma ya maji kabisa,badala yake wananchi wa kijiji hicho walikuwa wakipata huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji wa zamani uliopo kijiji cha Mkeke.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake Paligia Luoga alisema,mradi huo utakwenda kusaidia kumtua mama ndoo kichwani,hata hivyo ameiomba Ruwasa kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji ili kupunguza msongamano wa watu kwenye vituo vilivyopo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.