Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amefanya ukaguzi wa kushitukiza katika mradi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea iliyogharimu zaidi ya milioni 202.
Mndeme amesema ameamua kufanya ukaguzi huo kutokana na Halmashauri ya Manispaa hiyo kuitelekeza nyumba hiyo tangu ilipokamilika na kufunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016
Amesema madai ya kutoanza kutumia nyumba hiyo kwa sababu ya kukosa uzio,hayana msingi kwa kuwa serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa nyumba hiyo.
“Jengo hili limejengwa kwa thamani kubwa sana,milioni 202 mheshimiwa Rais angeweza kujenga zahanati mbili kubwa na kununua madawa,pia Mheshimiwa Rais kwa kutumia fedha hizo angeweza kujenga wadi mbili za mama na mtoto,lakini Rais aliamua kutoa fedha hizi ili Mkurugenzi apate makazi’’,alisisitiza.
Hata hivyo Mndeme amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma,kufanya uchunguzi ili kuona thamani ya fedha iliyojenga jengo hilo,mwaka 2016 kama zimetumika kwa usahihi.
Mkuu wa Mkoa amesikitishwa na kitendo cha jengo hilo kutotumika tangu kukamilika kwake miaka minne iliyopita ambapo amesisitiza madai ya kusema nyumba haijaanza kutumika kwa sababu hakuna uzio hayana msingi.
“Ni watu wangapi wanaishi na kufanyakazi katika nyumba ambazo hazina uzio,ninyi kama Manispaa kama kigezo muhimu ni nyumba kuwa na uzio mlitakiwa kuchukua hatua mapema’’,alisema Mndeme.
Hata hivyo amesema uzio ungeweza kuwekwa wakati mtu anaendelea kuishi ambapo ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kuhamia kwenye nyumba hiyo.
Amezuia fedha nyingine isitumike kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo na kwamba ameagiza kiasi cha shilingi milioni 20 iliyotengwa kwa ajili ya uzio, asiwekwe Mkandarasi badala yake uzio ujengwe kwa kutumia force account.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Philipo Beno amesema mradi huo ulitekelezwa kwa awamu nne ambapo awamu ya kwanza hadi ya tatu ilijengwa na Mkandarasi Shada Investiment co.Ltd na awamu ya nne ilijengwa na Mkandarasi MS AMU Communication Ltd.
Kwa mujibu wa Beno,Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na kukabidhiwa Manispaa ya Songea Julai 4,2017.
“Changamoto iliyosababisha nyumba hii kutokaliwa hadi sasa ni kutokuwa na uzio,lakini katika bajeti yetu ya mwaka 2018/2019,tuliweka bajeti ya ruzuku toka serikali kuu kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia uzio,ambayo hatukuipata’’,alisema Kaimu Mkurugenzi.
Hata hivyo amesema katika bajeti ya Manispaa inayoanzia Julai mwaka huu wametenga kiasi cha shilingi milioni 20 ili kujenga uzio huo.
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI MKOA WA RUVUMA
MEI 29,2020
SONGEA
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.