MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekemea mahubiri yanayoleta chuki na kuhatarisha amani na utulivu uliopo nchini.
Kanali Thomas ameyasema hayo wakati anazungumza na viongozi wa Taasisi mbalimbali za kidini mkoani Ruvuma kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Amewaasa viongozi wa dini kushirikiana na kuacha kudharauliana badala yake kujenga umoja wa madhehebu ya dini na kuzungumzia changamoto na mafanikio waliyonayo kwa manufaa ya watanzania wote.
“Katika mahubiri yenu msisahau kuliombea Taifa letu,siasa zisiwagawe viongozi wa dini,tuangalia kwanza nchi yetu ya Tanzania,msikubali kuliingiza Taifa kwenye matatizo kisa Imani ya dini au vyama vya Siasa’’,alisisitiza RC Thomas.
Amesisitiza kuwa Tanzania ni moja na kamwe haiwezi kugawanyika kwa sababu ya migogoro ya kidini au kisiasa ambapo pia amewaomba viongozi hao wa dini kuimarisha malezi bora kwa vijana na ili kuwa na Taifa lenye maadili mema.
Ametahadharisha kuwa ndoa nyingi zinavunjika kwa vijana ambapo amesema vijana wengi wanaingia kwenye ndoa bila kufanya maandalizi ya kutosha na kukosa mafundisho ya ndoa kutoka kwa viongozi wa dini.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza wazazi na walezi ambao bado hawajawapeleka Watoto wao shule wafanye hivyo mara moja.
Amesema kwa Watoto wanaosoma shule za serikali wanasoma bila ada na kwamba hata kama mtoto hana sare za shule wazazi na walezi wahakikishe wanampeleka mtoto shule.
Akizungumza kwenye kikao hicho Askofu Noel Mbawala wa Kanisa la Upendo Masihi KIUMA wilayani Tunduru ameipongeza serikali kwa kukemea mahubiri yaliyokuwa yanaleta uchochezi.
Amesema ili kuweka mahusiano mema Taasisi ya KIUMA imeajiri watumishi wengi waislamu ili kuwa na amani na uhusiano ulio mwema ambapo ametoa wito kwa Taasisi nyingine za kidini kuiga mfano huo.
Hata hivyo ameiomba serikali kuchukua hatua kwa vijana ambao wanatembea nusu uchi ambapo amedai msako wa kuwaondoa akina dada poa kutoka jijini Dar es salaam,wale akina dada wamerudi mikoani ambako wanaendeleza vitendo hivyo.
Amemuomba Mkuu wa Mkoa kwa kusaidiana na viongozi wa dini kuwakusanya akinadada hao ambao amedai wameingia mkoani Ruvuma ili kukaa nao na kuangalia namna ya kuwawezesha ikiwemo kuwapa mitaji midogo na kupewa elimu ya biashara ili waaache biashara haramu ya kujiuza.
Viongozi hao wa dini wamemuomba Mkuu wa Mkoa kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika baadhi ya mitaa mjini Songea, kudhibiti mgawo mkali wa maji eneo la Misufini Mshangano na mlundikano wa takataka katika eneo la Bombambili mjini Songea.
Mkuu wa Mkoa ameahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote ambazo wamezieleza ambapo amesema serikali ipo tayari kuendeleza ushirikiano na madhehebu ya dini ili kuwaletea maendeleo ya kimwili na kiroho.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anaendelea na ziara ya kukutana na makundi mbalimbali ili kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.